Majaliwa: Kamati za maafa za mikoa, wilaya Tanzania zipambane na corona

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameendesha kikao cha kamati ya kitaifa cha kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma na kutoa maagizo kadhaa ikiwamo la kamati za maafa za mikoa na wilaya kuungana katika mapambano ya kuzuia kuenea kwa corona nchini humo.

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameziagiza kamati za maafa katika ngazi za mikoa na wilaya ziungane na waratibu wa kupambana na virusi vya ugonjwa wa corona (COVID-19) waliopo katika maeneo yao.

Pia, Majaliwa amewasisitiza Watanzania waendelee kujikinga na ugonjwa huo kwa kuhakikisha wanajiepusha na misongamano isiyokuwa ya lazima na hata wakienda kwenye maeneo ya kutolea huduma kama sokoni, vituo vya mabasi wapeane nafasi kati ya mtu mmoja na mwingine.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana Alhamisi, Machi 26, 2020 wakati akiongoza kikao cha kamati ya kitaifa cha kukabiliana na corona ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma.

Kikao hicho kilihusisha wajumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Majaliwa aliagiza wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto ipeleke wataalamu katika maeneo yenye mahitaji makubwa kama kwenye viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na bandarini.

“Lengo letu ni kuhakikisha nchi inabaki salama hivyo Watanzania tuendelee kuwa na tahadhari ya kutosambaa kwa ugonjwa huu na pale tunapokwenda kwenye maeneo ya kutolea huduma tujipe nafasi kati ya mtu mmoja na mwingine,” alisema Majaliwa

Alisema kamati hiyo inatakiwa ifuatilie na isimamie vizuri ili kuhakikisha watu wote wanaoingia nchini wanapimwa na wanafuatilia ili kujua historia zao za safari katika kipindi cha siku 14, lengo likiwa ni kuzuia maambukizi hayo yasisambae kwa jamii.

Alisema watu wote waliopewa dhamana ya kuratibu shughuli ya kupeleka watu walioko kwenye karantini, wahakikishe wahusika wanafika kwenye hoteli walizozichagua.

Pia, Serikali inafanya utaratibu wa kutenga maeneo ambayo watu watakuwa wanakaa bila gharama na yatakuwa na huduma zote muhimu.

Pia, Waziri Mkuu amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona, ambapo amevitaka viendelee na utaratibu huo kwani utasaidia wananchi kupata elimu na kuweza kujikinga na maabukizi hayo.

Machi 23, 2020, Waziri Mkuu aliunda kamati tatu kwa ajili ya kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi ya corona (COVID-19).

Kamati hizo ni ya Kitaifa ambayo inaongozwa na Waziri Mkuu na itahusisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Wengine ni Waziri Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Pia, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Msemaji Mkuu wa Serikali, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali wa Tanzania na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika kikao cha jana, Waziri Mkuu ameongeza wajumbe wawili ili waongeze nguvu katika kukabiliana na virusi vya corona ambao ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.