Majaliwa: Mtumishi asiyefuata maadili hatufai

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mtumishi wa umma asiyetaka kufuata maadili ya utumishi pamoja na maelekezo ya viongozi wake hafai kufanya kazi serikalini.

Tanga. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mtumishi wa umma asiyetaka kufuata maadili ya utumishi pamoja na maelekezo ya viongozi wake hafai kufanya kazi serikalini.

Aliyasema hayo jana jioni Alhamisi Machi 5, 2020 wakati alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Korogwe na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa TTC Korogwe akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Tanga. 

Waziri Mkuu amesema uaminifu na uadilifu ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na watumishi wa umma nchini, hivyo aliwataka watumishi hao wasijiingize kwenye mambo ambayo hayana tija katika utumishi wao.

Amesema Serikali inataka kila mtumishi wa umma nchini awajibike kwa kufanya kazi kwa bidii na kufuata maadili ya kiutumishi na kwamba haitomvumilia mtumishi ambaye ni mwizi, mbadhirifu, mvivu na haitosita kumchukulia hatua.

“Watumishi mnatakiwa muwahudumie wananchi bila ya ubaguzi wa aliyenacho na asiyekuwa nacho kwa sababu wananchi wote wana haki sawa ya kuhudumiwa, hivyo hakuna sababu ya kuwabagua,” amesema Majaliwa.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Kasongwa ahakikishe anawasimamia wakuu wa idara katika kupanga ratiba za kwenda vijijini kuwasikiliza wananchi na kushirikiana nao katika kutatua kero zinazowakabili.

Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, Majaliwa amesema  Serikali ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo hilo na kuwataka wananchi waendelee kuwa na subra wakati suala hilo linashughulikiwa.

Amesema  kupitia Kampeni ya Rais John Pombe Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao. 

Kuhusu suala la upatikanaji wa umeme, Waziri Mkuu alisemamaeneo yote nchini yakiwemo ya wilaya ya Korogwe yatasambaziwa umeme kupitia Mradi wa Nishati Vijijini (REA).

Alisema wakati wa usambazaji wa huduma hiyo wananchi hawatowajibika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

“Rais wetu anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama ya Sh27,000 tu,” amesema.

Naye mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava na wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda wameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya, elimu na pia waliiomba iwasaidie katika kutatua changamoto ya barabara, maji na umeme.

Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi kwenye mradi wa shamba la ufuta Mkomazi na kujionea miundombinu ya umwagiliaji. Pia, alizindua miradi ya ghala la kuhifadhia nafaka Mombo na alifungua maktaba ya chuo cha ualimu Korogwe.