Majaliwa, Ndugai walivyozungumzia bungeni kero ya bei za maji

Thursday September 12 2019

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma.  Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amekerwa mamlaka za maji nchini humo kupandisha bei za maji kwa kiasi kikubwa.

Ndugai ameonyesha kukerwa leo Alhamisi Septemba 12, 2019 wakati wa kipindi cha maswali ya papo bungeni kwa hapo kwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mariam Kisangi amesema kumekuwa na changamoto ya kupanda kwa bei za maji, ankara zisizo sahihi na kukosa maji kwa muda mrefu kisha kuletewa ankara kubwa.

“Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi wake waliokumbwa na kero hiyo?” amehoji.

Akijibu, Majaliwa amesema zipo mamlaka zinapandisha bei za maji kupita kiasi na kutoa mfano wa malalamiko yake aliyoyapata wakati akiwa ziara wilayani  Maswa Mkoa wa Simiyu ambapo bei ya maji imeongezeka kutoka Sh5,000 hadi Sh28,000.

“Sasa bei hizi hazina uhalisia. Hakuna sababu ya mamlaka kutoza fedha zote hizo na kuwafanya ili wananchi wakose maji. Serikali ndio inatekeleza miradi hii ili kuwafanya wananchi wapate maji,” amesema.

Advertisement

Amesema hawapaswi kutoza fedha hizo wala hawapaswi kurudisha gharama za mradi kwa sababu Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kupata maji.

Amesema Serikali haijadai fedha kwa ajili ya miradi hiyo na kwamba juzi alikuwa na Waziri wa Maji  na alimweleza kuhusiana na jambo hilo.

“Bei ambazo zinatakiwa kuwekwa ni zile ambazo wananchi wa kule kijijini anaweza kuzimudu lakini si kwa kuweka Sh5,000 hadi Sh28,000 ni jambo ambalo halina uhalisia,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia mamlaka za maji na kuendelea kutoa huduma za maji kwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji chini ya mamlaka hizi.

“Lakini hatutaruhusu Mtanzania kutozwa gharama kubwa maji kiasi hicho huku tukitoa wito ni lazima tuchangie huduma hizi ili tuweze kununua dizeli,” amesema.

Amesema katika kupandisha bei ni lazima Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na wadau wengine washirikishwe kabla ya kupandisha bei hizo.

Ndugai amesema jambo hilo ni kero kweli, “Mtu alikuwa analipa bill (ankara) ya Sh10 leo analetewa bill ya Sh80,000 nyumba ile ile watu ni wale wale na hii ni ya nchi nzima.”

Advertisement