Majaliwa aagiza mkurugenzi bodi ya mkonge kurudishwa alikotoka

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza mkurugenzi wa bodi ya mkonge Tanzania, Yunus Mssika kurudishwa wizara aliyotoka na nafasi itakaimiwa na katibu wa timu ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali katika tasnia ya kilimo cha mkonge mkoani Tanga, Saddy Kambona.

Tanga. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza mkurugenzi wa bodi ya mkonge Tanzania, Yunus Mssika kurudishwa wizara aliyotoka na nafasi itakaimiwa na katibu wa timu ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali katika tasnia ya kilimo cha mkonge mkoani Tanga, Saddy Kambona.

Pia, amewasimamisha wajumbe wote wa bodi ya mkonge hadi hapo watakapotaarifiwa, lengo ni kuhakikisha zoezi la urejeshaji wa mali linafanyika kwa ufanisi.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Machi 6, 2020 alipokutana na bodi ya mkonge  katika kikao kilichofanyika mjini Tanga.

Katika kikao hicho katibu wa timu ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali katika kilimo cha mkonge Tanga aliwasilisha taarifa ya mali za iliyokuwa Mamlaka ya Mkonge ambazo zilitumika kinyume na taratibu na zinatakiwa zirejeshwe serikalini.

Baada ya taarifa hiyo, Majaliwa amesema ili utaratibu wa kurejesha mali hizo utekelezeke kwa ufanisi ni mkurugenzi kurudishwa  katika wizara aliyotoka na wajumbe wa bodi ya mkonge  wakasubiri hadi hao watakapotaarifiwa.

Amesema Kambona anaanza zoezi la kuratibu na kuishauri timu katika shughuli ya urejeshwaji wa mali na ndiye atakayesimamia shughuli za bodi.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa mwenyekiti wa bodi ya mkonge Tanzania Mariam  Nkumbi ataendelea na majukumu yake.

“Watachukua hatua kwa watu wote waliohusika na upotevu wa mali zote na kwamba maamuzi hayo yamefanyika ili kuzua uvurugwaji wa muundo wa uchunguzi wa kwa sababu mali ni nyingi n azote zinatakiwa zirejeshwe Serikalini,” Amesema Majaliwa.

Amesema Serikali inataka kuona jambo hilo linaenda bila ya kusimama na mali zote zinarudi mikononi mwa bodi.

Machi Mosi, 2020 Majaliwa alipokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali katika kilimo cha mkonge mkoani Tanga na kuagiza mapendekezo yaliyotolewa na timu hiyo yakiwemo ya kurejeshwa serikalini kwa nyumba namba 176 eneo la Bombo ambayo ilimilikishwa kwa Salum Shamte,  yafanyiwe kazi.

Nyumba nyingine zilizopendekezwa kurejeshwa serikalini ni pamoja na nyumba 10 zilizoko ndani ya Jiji la Tanga katika maeneo ya Raskazone, Bombo, Nguvumali na Market street ambazo zilinunuliwa na watumishi hao kwa udanganyifu.

Timu hiyo maalum ya uchunguzi iliundwa na Majaliwa  na ilifanya uchunguzi mkoani Tanga kuanzia tarehe Novemba 29, 2019 hadi Februari 7, 2020. Timu hiyo iliyokuwa na  wajumbe 13 ilihusisha maofisa kutoka ofisi mbalimbali za Serikali.

Uchunguzi huo maalum ulihusu masuala mbalimbali ya zao la mkonge mkoani Tanga ambayo ni pamoja na uzalishaji wa mkonge, bei ya zao la mkonge katika soko la ndani na nje ya nchi.

Pia, ilichunguza kuhusu mali za iliyokuwa Mamlaka ya mkonge nchini, ubia kati ya Kampuni ya Katani Limited na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Utendaji kazi wa Kampuni ya Katani Ltd na pia utendaji kazi wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB).