VIDEO: Majaliwa aagiza watumishi watatu walioajiriwa ‘kindugu’ kuondolewa kazini

Muktasari:

Panga la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa limeendelea kuondoka na vichwa vya watumishi kupitia ziara yake katika Mikoa na halmashauri mbalimbali nchini huku akiacha maagizo kuhusu udhaifu aliokutana nao.

Dar es Salaam. Panga la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa limeendelea kuondoka na vichwa vya watumishi kupitia ziara yake katika Mikoa na halmashauri mbalimbali nchini huku akiacha maagizo kuhusu udhaifu aliokutana nao.

Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi Manispaa ya Singida, Bravo Lyapembile leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 kuwaondoa kazini watumishi watatu wanaokusanya mapato kwenye stendi ya mabasi, ambao inadaiwa wameajiriwa kindugu na wanatumiwa kuiba mapato.

Agizo hilo amelitoa wakati akizungumza na madiwani, watumishi wa Manispaa ya Singida pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Singida kupitia mkutano uliofanyika ukumbi wa Roman Catholic, mjini Singida.

Majaliwa aliwataja vijana hao waliowekwa kindugu ni Kennedy Francis (mtoto wa Mkurugenzi), Selemani Msuwa (ndugu yake diwani) na Salehe Rajab Kundya (shemeji yake diwani mwingine).

“Andika barua leo hii hawa vijana waondoke kwenye hiyo kazi, na upeleke timu nyingine ya watu waaminifu, kuna mchezo unachezwa wa kukusanya mapato lakini hayapelekwi benki na wahusika wakuu ni mweka hazina wa Manispaa, Aminieli Kamunde na Mkaguzi wa Ndani, Ibrahim Makana, ” amesema Majaliwa akimuagiza Mkurugenzi huyo Lyaembile.

Majaliwa ametoa onyo watendaji wa kata wanaohusika kukusanya mapato kupeleka fedha hizo benki na kupatiwa risiti, akilaani wakusanyaji wanaoshirikiana na baadhi ya Wakurugenzi na Waweka Hazina.

Katika ziara hiyo, pia Majaliwa amekemea tabia aliyoikuta Halmashauri nyingine ya kubadilisha matumizi ya fedha, akiwataja Mkurugenzi au Mweka Hazina kuwadai watendaji wa kata wawapatie Sh2milioni. Majaliwa amewataka kupeleka fedha benki na kupatiwa risiti.

Tabia nyingine iliyomshangaza Majaliwa ni pamoja na kubadilishwa kwa matumizi ya fedha na kuacha malengo kusudiwa ya fedha zilizotumwa.

 “Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, simamieni mapato ya ndani na siyo muwe sehemu ya ulaji wa fedha za umma. Madiwani simamieni sheria inayosimamia utoaji wa asilimia 10 ya mapato kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu ili kila mmoja apate haki yake,” alisisitiza.

 

Aidha, Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida, Rashid Mandoa kukamilisha malimbikizo ya madiwani yanayokadiriwa kufikia Sh104milioni.

Majaliwa amemtaka awasilishe kwenye mfuko wa Hifadhi ya jamii, michango ya madereva wanayokatwa tangu mwaka 2015/2016. Amesema madereva hao hukatwa ila michango yao haipelekwi katika mfuko huo.

“Watu hao pia wamekuwa wakikatwa sh5,500 za Bima ya Afya tangu wakati huo lakini hadi sasa michango yao haijawasilishwa na matokeo yake wakienda hospitali hawatibiwi. Hakikisha malipo yao yanaenda,” amesema.