Majaliwa ahoji aliyemhamisha kuendelea na kazi

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa barabara ya muda kwenye eneo la daraja la Kiyegeya na kusema kazi inaenda vizuri sababu hakuna tena msongamano wa magari kama ilivyokuwa wiki iliyopita.

Morogoro. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa barabara ya muda kwenye eneo la daraja la Kiyegeya na kusema kazi inaenda vizuri sababu hakuna tena msongamano wa magari kama ilivyokuwa wiki iliyopita.

Majaliwa amesisitiza kuwa mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wa mikoa yote nchini wanapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa madaraja yote siyo kwa juu tu bali hadi chini ya madaraja ili kujiridhisha na usalama wake.

“Nilitoa agizo kwa mameneja wa Tanroads ambao wana highways, wazikague kila mara kwa sababu hatuhitaji kuwa na highways zilizobomoka,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumanne, Machi 10, 2020 wakati akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na viongozi wa Mkoa wa Morogoro, mara baada ya kutembelea eneo hilo na kukagua ujenzi wa barabara ya muda ili kurejesha mawasiliano na mikoa mingine.

“Nimekuja kuona kazi inaendeleaje, nimekuta msongamano wa magari hakuna kama ilivyokuwa wiki iliyopita. Ile diversion (barabara ya mchepuko) imesaidia kuondoa msongano uliokuwepo,” amesema Waziri Mkuu.

“Mahitaji yetu ni kuwa na daraja la kudumu, kwa hiyo mharakishe ujenzi wa daraja hilo, Mmesema sasa hivi mnapanga kuweka daraja la zege ili maji yakija kwa wingi yaweze kupita juu ya hii barabara ya muda, msisitizo ni kukamilisha kazi ya daraja la kudumu,” amesema wakati akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale.

Katika ukaguzi huo, Waziri Mkuu alibaini kuwa Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Godwin Andalwisye ambaye aliagiza arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine, bado alikuwepo kwenye eneo la tukio akiendelea na kazi.

“Uamuzi niliochukua wa kumhamisha Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro ulikuwa sahihi kwa sababu huyu anaonekana hawezi kazi ya kusimamia wengine. Fedha ya ukaguzi ipo, ya ujenzi ipo, halafu kazi haifanyiki. Kazi ya kusupervise haiwezi, kwa hiyo, ateuliwe meneja mwingine.

“Nilimuuliza meneja aliyekuwepo kama wana fedha za ukaguzi, akasema anayo. Nikamuuliza kama anayo fedha ya spot maintenance, akasema anayo. Fedha hizi zote zilipaswa zitumike kwa kazi iliyopangwa, lakini hilo halikufanyika,” amesema Majaliwa.

Akijibu hoja hiyo, Mfugale alisema amemuacha Andalwisye aendelee kuwepo kwa  sababu ya utalaamu wake kwenye madaraja. “Ulishatoa maelekezo kuwa aondolewe, na wa kumhamisha ni mimi, tunatumia tu utaalamu wake.”

Alipoulizwa kama ameshateua meneja mwingine wa Mkoa wa Morogoro, Mfugale alikiri kwamba bado hajamteua mtu mwingine.

Jumatano iliyopita, Machi 4, 2020, Majaliwa alikatisha ziara yake mkoani Tanga na kutembelea eneo hilo ambako alishuhudia mlundikano wa magari na abiria hali ambayo haikumfurahisha.

Aliagiza Andalwisye arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine mara moja kwa sababu ya kuzembea kutimiza wajibu wake.

Waziri Mkuu ambaye alisafiri kwa magari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, pia alisimama Morogoro na kukagua ujenzi wa uzio wa makaburi ya Kola Hill ambako walizikwa wahanga wa ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kulipuka Agosti 10, 2019 na kuua watu 115, kati yao wanaume walikuwa ni 109 na wanawake ni sita.

Akiwa makaburini hapo, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Morogoro uweke utaratibu wa kuwa na mtu maalum atakayesimamia masuala ya mazishi yote yatakayofanyika kwenye makaburi ya Kola Hill.

Amesema mtu huyo ahakikishe makaburi yote yanachimbwa katika utaratibu na mpangilio utakaoliwezesha eneo hilo kuwa na nafasi ya kuzika watu wengi. “Utaratibu wa sasa wa kuchimba makaburi kiholela utalifanya eneo hili lijae haraka huku likiwa halina mpangilio maalum.”

Waziri Mkuu pia aliridhia maombi ya uongozi wa mkoa wa Morogoro ya kutaka akubali makaburi hayo yajengewe ili yawe na mwonekano mzuri kazi ambayo itagharimu zaidi ya Sh12 milioni.

Uongozi huo pia uliomba rdhaa ya Waziri Mkuu kutengeneza mandhari ya ndani ya uzio (Landscaping) kazi ambayo itagharimu Sh1,682,500  pamoja na kujenga mnara wa kumbukumbu kwa gharama ya Sh 4,173,125.