Majaliwa amjibu kwa vitendo Mizengo Pinda

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amefungua mkutano wa mwaka wa Wadau wa Lishe huku akipokea mapendekezo ya mtangulizi wake kwenye nafasi hiyo, Mizengo Pinda.

Dodoma. Mapendekezo manne yaliyotolewa na waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, Mizengo Pinda ya kupambana na lishe yamepokelewa na Serikali nchini humo na kuanza kuyatekeleza.

Mapema leo Alhamisi Oktoba 3, 2019 katika mkutano wa wadau wa lishe jijini Dodoma, Pinda alimwomba Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kubeba mambo manne na kuyafanyia kazi ikiwemo kuwatumia wasanii, wanahabari, ujumbe katika mwenge na ilani za vyama ili kuishinda vita ya lishe.

Akifungua mkutano huo muda mfupi baada ya ombi hilo, Majaliwa amesema mawazo ya Pinda ni mazuri hivyo atayafanyia kazi.

"Kwa kuanza hapa leo napendekeza kikundi hiki kilichotumbuiza (Kikundi cha ngoma za kigogo cha Nyota) watakwenda Lindi Oktoba 14, 2019 katika kilele cha mbio za Mwenge lakini ninyi mbebe ujumbe wa lishe," amesema Majaliwa huku akiwazawadia wasanii hao Sh100,000.

"Watanzania tumekuwa na mtazamo mbaya kwamba mtu akiwa na kitambi ndiyo anaonekana kuwa bora lakini kinyume chake mtu anaonekana hafai, hasa tatizo la vitambi liko kwa wasomi walioko makazini,"

Waziri Mkuu amesema utapiamlo bado ni janga nchini Tanzania licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na wataalam hivyo akazitaka taasisi kuwa makini na kuiambia serikali katika mapungufu ya sera ili yaweze kuondolewa na kuwepo na matokeo ya chanya.

Ameziagiza wizara zote, wadau wa maendeleo na asasi za kijamii kutenga fedha kwa ajili ya lishe na kutumia mapendekezo yote yanayounga mkono mapambano ya  vita hiyo pamoja na kutumia vyombo vya habari.

Majaliwa amesema ni muhimu elimu ya lishe ikatolewa kwa wananchi wote.

“Pamoja na tafiti kuonesha kwamba tumepunguza viwango vya udumavu na upungufu wa damu bado viwango vyake havikubaliki kimataifa. Vilevile, tuna viwango vya utapiamlo ambavyo vimezidi kuongezeka na havikubaliki kimataifa ikiwemo uzito uliozidi kwa wanawake wenye umri wa kuzaa,” amesema

 

Awali, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndungulile alisema udumavu umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2015 na kufikia asilimia 31.5 mwaka huu.

Dk Ndungulile alisema licha kupungua kwa udumavu, changamoto iliyopo kwa sasa ni suala la unyonyeshaji kwa watoto walio na umri wa chini ya miezi sita, wanaonyenyeshwa ni asilimia 58 tu, huku asilimia 30 ya Watoto wenye umri wa zaidi ya miezi sita hawalishwi vizuri.