Majaliwa aongoza mazishi ya Alhaj Zingizi, atoa nasaha

Muktasari:

Mfanyabiashara na mwanazuoni maarufu wa dini ya Kiislam, Alhaj Aziz Massanga (Zingizi) aliyefariki Jumatano ya Novemba 27, 2019 jijini Johanesburg nchini Afrika Kusini  amezikwa jana Ijumaa Novemba 29, 2019 katika makaburi ya Msasani, Dar es Salaam nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameongoza wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine kwenye mazishi ya mfanyabiashara na mwanazuoni maarufu wa dini ya Kiislam, Alhaj Aziz Massanga (Zingizi), yaliyofanyika katika makaburi ya Msasani.

Alhaj Zingizi amefariki dunia Jumatano ya Novemba 27, 2019 jijini Johanesburg nchini Afrika Kusini  alikokwenda kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Marehemu Alhaj Zingizi alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya kibofu.

Akizungumza baada ya mazishi hayo yaliyofanyika jana jioni Ijumaa, Desemba 29, 2019, Majaliwa aliwaasa wananchi kumuenzi marehemu Alhaj Zingizi kwa kufanya mambo mema kama alivyokuwa akiyafanya enzi za uhai wake. “Marehemu Zingizi alikua ni mtu mwenye kusaidia jamii kwa hali na mali.”

“Marehemu ametenda mengi mema katika msikiti wake na jamii iliyomzunguka. Alisaidia wenye mahitaji, hivyo na sisi hatuna njia nyingine ya kumuenzi marehemu bali ni kutenda mema kwa jamii hususani kwa kuwajali watu wenye shida ili wale waliokua wananufaika wasione pengo kubwa,” alisema Majaliwa

Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali ipo pamoja na viongozi wote wa dini na wala wasisite kuijulisha pale wanapopatwa na jambo lolote ipo tayari kushirikiana nao kwa namna moja au nyengine.