Majaliwa asema elimu ya sasa haina msaada kwa vijana wanaomaliza vyuo

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema mitalaa inayotumika katika elimu nchini humo haiwasaidii vijana katika soko la  ajira huku akisema umefika wakati ikapitiwa upya.

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ni wakati sasa kwa Serikali kuipitia upya na kuhuisha mitalaa ya elimu kwani iliyopo haiwasaidii vijana kujiajili.

Akizungumza leo Ijumaa Septemba 20, 2019 katika kongamano la Kitaifa la Ushiriki wa Watanzania katika miradi ya Kimkakati, mafanikio, fursa na changamoto lililofanyika jijini Dodoma, Majaliwa amesema elimu ya sasa haina msaada kwa vijana wanaomaliza vyuo.

"Kijana anasoma historia halafu akimaliza huyu unategemea akapate wapi ajira, hili litazamwe upya," amesema Majaliwa

Waziri Mkuu amesema ni wakati wa kuangalia jinsi ya kuwasaidia vijana ili watakapomaliza elimu kwa ngazi yoyote waweze kuajilika.

Kwa upande mwingine, Majaliwa amekaribisha tafiti za wasomi kuwa lazima zichukuliwe kwa uzito na serikali iwape nafasi kwani baadhi zinakuwa ni msaada mkubwa kwa taifa.