Majaliwa asema uhusiano Tanzania, Afrika Kusini ulichangia kumaliza ubaguzi wa rangi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Rais wa Afrika Kusini, Cyrill Ramaphosa zawadi ya picha tente ujumbe wa mpigania uhuru wa nchi hiyo, Solomon Mahlangi, wakati Ramaphosa alipotembelea eneo la iliyokuwa kambi ya wapigania uhuru wa nchini hiyo la Mazimbu ambalo kwa sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu ya Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mkoani Morogoro, leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa azungumzia uhusiano wa Afrika Kusini na Tanzania na kueleza kuwa umoja baina ya nchi hizo utasaidia kuvuka changamoto wanazokabiliana nazo.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Afrika Kusini umekuwa chachu ya kushirikiana katika majukwaa ya kimataifa hususan kupambana na ubaguzi wa rangi ambao ulikuwa umekithiri.

Kadhalika amesema Serikali zote zinatambua ni umoja pekee utakaowezesha kuvuka vizingiti na changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi hizo.

Majaliwa ameyasema hayo leo Ijumaa Agosti 16,2019 katika Chuo cha Solomon Mahlangu kilichopo Mazimbu Morogoro nchini Tanzania wakati wa ziara ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.

Amesema nchi hizo zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kihistoria ambao umechagizwa na eneo la Mazimbu ambalo lilitumika kama kituo cha wapigania uhuru wa Afrika Kusini kujifunza namna ya kupambana.

“Mazimbu ni eneo lenye historia na linaonyesha uhusiano wa kihistoria baina ya nchi zetu mbili. Huwezi kuelezea uhusiano wa kihistoria kati ya Afrika Kusini na Tanzania bila kuitaja Mazimbu.”

“Tunapoongelea kukoma kwa sera za ubaguzi wa rangi Afrika Kusini daima tutawakumbuka Mwalimu Nyerere na Mzee Mandela kwa sababu ya utumishi wao wa kujenga misingi imara ya umoja na mapambano dhidi ya ubaguzi,” amesema Majaliwa

Majaliwa amesema namna pekee ya kuwaenzi viongozi hao ni kuendelea kuujenga umoja kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi yetu

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako amesema wizara yake na Serikali kwa ujumla itakuwa tayari kutoa msaada wowote kutimiza dhamira hiyo ya Kiswahili kuanza kufundishwa nchini Afrika Kusini.