Majaliwa ataka aliyekamatwa na zana za uvuvi haramu Mwanza kuchukuliwa hatua

Muktasari:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Mwanza kumchukulia hatua za kisheria mfanyabiashara aliyekamatwa kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya zana haramu za uvuvi.

Mwanza. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Mwanza kumchukulia hatua za kisheria mfanyabiashara aliyekamatwa kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya zana haramu za uvuvi.

“Yuko mfanyabiashara anaitwa Jeremiah Asam Omolo amekamatwa mara kadhaa kwa kukutwa na nyavu haramu. Wizara ilitoa aina ya nyavu zinazoruhusiwa kutumika na kamati  ya Mkoa ikasimamia lakini kuna maofisa wa Wizara waliingilia zoezi hilo mara tatu na akatozwa faini mara zote,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumatano Aprili 15, 2020 wakati akizungumza na kamati hiyo kwenye kikao alichokifanya kwa njia ya video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

“Mkuu wa Mkoa aliunda timu ya kuchunguza matukio haya. Hii ni timu ya Serikali na imeaminiwa kufanya kazi hii, na ina uwezo wa kuchukua hatua. Lazima kamati ya Mkoa isimamie na ichukue hatua. Hatuwezi kuwa na Wizara ambayo haiiamini kamati  ya Mkoa,” amesisitiza.

Amesema hatua pekee ambazo zilichukuliwa na Wizara ni kumtoza faini mfanyabiashara huyo kwa kumlipisha zaidi ya Sh470 milioni.

“Lengo la Serikali siyo kutoza fedha peke yake, bali ni kudhibiti matumizi ya nyavu haramu nchini,” amesisitiza.

Amesema kwa kuwa si mara yake ya kwanza kukamatwa, kamati ya Mkoa haina budi kuchukua hatua kali zaidi kwa sababu nia ya kutoa adhabu ni kumfanya mkosaji asirudie kosa lakini mfanyabiashara huyo amekuwa akilipa faini na kurudia makosa yaleyale.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema  katika kosa la kwanza, mfanyabiashara huyo alipatikana na marobota 66 ya nyavu haramu aina ya makila sawa na vipande 13,200 ambapo alitozwa faini ya Sh50 milioni.

Amesema katika tukio la pili la Aprili 3, 2020  Omolo alikutwa na zana haramu za uvuvi aina ya makila vipande 6,964 na timba vipande 179 na kutozwa faini ya Sh129.8 milioni.

“Katika tukio la tatu Aprili 4, 2020 alipatikana na kosa la kumiliki zana haramu za uvuvi ambazo ni marobota 10 ya nyavu haramu aina ya makila sawa na vipande 300 na marobota 437 ya nyavu haramu aina ya Timba sawa na vipande 12,875 na kutozwa faini ya Sh300 milioni,” alisema.

Alisema uongozi wa mkoa uliamua kuunda timu ya wataalamu inayojumuisha vyombo vya usalama ambayo itafuatilia na kuchunguza kwa undani mienendo ya mtuhumiwa huyo ikiwemo masuala la kikodi na ufanyaji wa biashara.

Mkuu huyo wa Mkoa alimweleza Waziri Mkuu kwamba timu hiyo iliyoundwa Aprili 9, 2020 itapaswa kukamilisha kazi yake na kukabidhi taarifa yake Jumatatu ijayo Aprili 20, 2020.

Majaliwa amekemea mikusanyiko inayofanyika kwenye nyumba za ibada kwa kigezo cha kutaka watoto wasikae majumbani kwa vile hawaendi shuleni.

“Ninazo taarifa kwamba wameanzisha mfumo wa kupeleka watoto kwenye madarasa ya dini maarufu kama Sunday School. Tumeruhusu ibada tu, na hizo ibada lazima ziangaliwe ziwe za muda mfupi kadri inavyowezekana. Tumesisitiza kwenye makanisa au misikiti ambako ibada zinafanyika, waumini wakae kwa kuachiana nafasi,” amesema.

Amesema changamoto inajitokeza kwenye makanisa makubwa ambayo yana waumini karibu 3,000.

“Hayo sasa yatakuwa ni makongamano. Tunaaamini Maaskofu na Mufti wataliweka vizuri suala hili la sunday school na madrassa,” amesema.

Amesema Serikali haitazuia biashara kwenye masoko, maduka makubwa isipokuwa amewataka wenye biashara hizo wahakikishe wanaweka ndoo za maji na sabuni ili wateja wanawe mikono kabla ya kuingia kupata huduma na wakati wanapotoka kupatiwa huduma hizo.

Kuhusu mikusanyiko mingine, Waziri Mkuu amesema watu wanapaswa wajizuie kwenda kuzagaa kwenye vituo vya mabasi na kama hawana shughuli za lazima za kufanya huko, basi wabakie majumbani kwao.