Majaliwa ataka biashara kati ya Tanzania na Urusi kuratibiwa

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameutaka ubalozi wa Tanzania nchini Urusi  kuratibu mipango ya wafanyabiashara wa nchi hiyo wanaotaka kuwekeza nchini.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameutaka ubalozi wa Tanzania nchini Urusi  kuratibu mipango ya wafanyabiashara wa nchi hiyo wanaotaka kuwekeza nchini.

Majaliwa ametoa agizo hilo jana Alhamisi Oktoba 24, 2019 baada ya kugundua uwepo wa wafanyabiashara wengi wa Urusi wanaotaka kuja Tanzania kuangalia maeneo ya uwekezaji pamoja na kutafuta wafanyabiashara wa Tanzania  watakaoungana nao katika uwekezaji wanaokusudia kuufanya.

“Tayari miadi imekwishawekwa ya kuwakaribisha wawekezaji wa Urusi kuja Tanzania kwa ushawishi wangu  pamoja na wafanyabiashara wa Tanzania, nisingependa wafanyabiashara hao wasumbuliwe au kukatishwa tamaa katika kutimiza nia yao hiyo,” amesema Majaliwa.

Amesema mkutano baina ya wakuu wa nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi uliomalizika jana Oktoba 24, 2019 ulilenga kujenga uhusiano mzuri zaidi katika nyanja mbalimbali hususani za kiuchumi.

Majaliwa amesema Urusi imeutumia mkutano huo kueleza bayana maeneo ambayo wapo tayari kushirikiana na Afrika katika kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na uuzaji wa zana za kilimo kama vile matrekta, sekta ya mafuta na gesi pamoja na madini, ujenzi wa miundombinu hasa reli, masuala ya elimu hasa utoaji wa nafasi za mafunzo nchini humo.

Amesema Tanzania imejinadi vizuri ikiongozwa na yeye mwenyewe kwa kufanya mazungumzo na viongozi wa kampuni zaidi ya nane za Urusi ili kuzishawishi ziwekeze nchini na zote zilikubali kuja Tanzania.

“Viongozi wa kampuni zote nilizopata  nafasi ya kuzungumza nazo wamesema wako tayari kuja nchini kufanya mazungumzo na Serikali pamoja na wafanyabiashara wazalendo ambao wako tayari kuungana na wafanyabiashara hao katika kuwekeza nchini Tanzania,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema viongozi hao walimueleza maeneo ambayo wanaamini kuwa wanafanya vizuri na wangependa kupata kibali cha kuwekeza Tanzania baada ya mazungumzo yao na Serikali, “pia walieleza ni kwa namna gani Taifa litanufaika na uwekezaji wao.”

Amebainisha kuwa tayari wafanyabiashara  18 wa Tanzania walijitokeza kushiriki mkutano huo na waliwapa habari wenzao wa Urusi kuhusu mazingira mazuri ya kuwekeza yaliyopo nchini.