Majaliwa ataka wakuu wa idara kuwafuata wananchi vijijini

Mafinga. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa  amewataka wakuu wa idara nchini kwenda kwa wananchi vijijini na kutoa elimu ya uraia kulingana na maeneo wanayoyasimamia badala ya kuwaachia wasio na utaalam.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Septemba 26, 2019 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri za Mufindi na Mji wa Mafinga Wilaya ya Mufindi katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.

Amesema mkuu wa kila idara katika Halmashauri zote nchini anapaswa kwenda kwa wananchi na kutoa elimu kuhusu shughuli  anayosimamia kwenye eneo lake.

"Fanyeni mikutano,  kila mkuu wa idara waelimisheni wananchi moja kwa moja na sio kujifungia ofisini. Wewe Ofisa elimu usiishie kwenye shule na kuzungumza na walimu au wanafunzi pekee, fanya mkutano na wananchi zungumza masuala ya elimu.”

“Mtu wa mazingira pia si hadi mwananchi aharibu mazingira ndio mnakwenda kuchukua hatua, mtu wa hospitali nenda vijijini katoe elimu kuhusu usafi wa mazingira ili kujikinga na magonjwa ya kuhara na sio kusubiri kipindupindu kitokee,” amesema Majaliwa.

Ameongeza, “Mkuu wa idara ndio mtaalamu wa eneo fulani, ndio  mhusika mkuu sio kumuachia diwani au mkuu wa wilaya kuelezea jambo kwa wananchi wakati hawana utaalamu nalo, badilikeni.”

Awali, mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amemueleza Majaliwa jinsi wanavyowasimamia watumishi katika Halmashauri kutimiza wajibu kwa wananchi kwa vile wapo kwenye vitengo hivyo kwa ajili ya kuwatumikia.

“Kila halmashauri, watumishi wapo hapo kwa sababu ya kuwatumikia  wananchi kwa usawa. Jukumu letu ni kuona tunawasimamia waweze ili kila mtumishi atimize wajibu wake na kutojiona  Mungu katika utumishi wake,” amesema Majaliwa.