Majaliwa atoa maagizo kwa DC Mtatiro waliokula fedha za korosho

Monday November 18 2019

 

By Irene Bwire, Ofisi ya Waziri Mkuu

Mtwara. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Julius Mtatiro ahakikishe anaondoka na Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho hadi Tunduru ili wakahakiki ni kwa nini wakulima hawajalipwa.

"Nimefurahi kusikia minada ya korosho inakwenda vizuri. Lakini sijafurahia habari ya Tunduru. Mheshimiwa Rais aliagiza Sh40 milioni zipelekwe kwa wakulima. Na ninajua kwamba zimeshalipwa. Sasa ni kwa nini wakulima bado wanadai?, amehoji.

"Ukitoka hapa kwenye mkutano nenda pale jengo la Bodi ya Korosho. Ondoka na Mtendaji Mkuu wake, mwende Tunduru akafuatilie ni kwa nini malipo ya mwaka jana hayajalipwa hadi sasa,” amesema Majaliwa

"Nataka afuatilie fedha zimekwama kwa nani. Kaimu Mkuu wa Mkoa ukigundua wanaokwamisha ni viongozi wa ushirika, shughulika nao hukohuko kama ambavyo umekuwa ukifanya," amesisitiza. Mtatiro pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru

Majaliwa ametoa agizo hilo leo mchana Jumatatu Novemba 18, 2019 wakati akifungua kongamano la siku moja la Wakandarasi na Wazabuni wa mikoa ya Kusini lilioandaliwa na benki ya CRBD kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) mjini Mtwara.

Akizungumzia kuhusu kongamano hili ambalo kaulimbiu yake ni "Pamoja nawe kukuza uchumi", Waziri Mkuu amewataka wakandarasi hao baada ya kupata elimu kidogo kuhusu shughuli za benki hiyo, anataraji kuwa wataenda kwenye Halmashauri zao na kutafuta kazi.

Advertisement

"Serikali inajenga miradi mikubwa kama vile bwawa la kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji la Mwalimu Nyerere, bomba la mafuta la kutoka Hoima hadi Tanga na miradi ya maendeleo kama ile ya barabara, reli, ujenzi wa  hospitali, madarasa na nyumba za walimu. Miradi yote hii inawatarajia ninyi wakandarasi mkaijenge."

Majaliwa ametumia fursa hii kutoa wito kwa viongozi na watendaji wazingatie utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa kutenga zabuni zenye thamani ya chini ya Sh10 bilioni kwa ajili ya wazabuni Watanzania ili kuwajengea uwezo na kushiriki katika zabuni. Amesema Serikali kwa upande wake itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, Abdulmajjid Nsekela kwa kubuni programu hiyo ya tofauti ambayo imelenga kuwainua wakandarasi wadogo na wa kati. 

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki qa kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,  Gelasius Byakanwa alisema hadi sasa jumla ya tani 67,000 za korosho zimeuzwa mkoani humo kupitia minada mitatu.

Oktoba 30, 2019 mnada wa kwanza ulipofanyika bei ilikuwa Sh2,468 kwa kilo na mnada wa  Novemba 15, 2019 ulishuhudia bei ikipanda na kufikia Sh2,890 kwa kilo.

Alisema katika msimu huu, korosho zimeingiza Sh1.75 bilioni  ambapo kati ya hizo, Sh1.20 bilioni  zimeshaingizwa kwenye akaunti na kupelekwa kwa wakulima.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa benki ya CRDB, Nsekela alisema bei hiyo inamsaidia mteja kwa kutoa ushauri, kumwezesha na  kushirikiana naye kuijenga nchi.

"Leo tuko Mtwara,  lakini tumeshaendesha makongamano kama haya katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza. Na hapa Mtwara tumejumuisha pia mikoa ya Lindi na Ruvuma," alisema.

Alisema benki hiyo ina hisa Sh6.3 trilioni ambazo ni sawa na asilimia 20 ya hisa za mabenki yote na kwa upande wa amana, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema amana za benki hiyo zinafikia Sh4.9 trilioni ambazo ni sawa na asilimia 23 ya amana za benki zote nchini.

Advertisement