Majaliwa aunda kamati tatu za kupambana corona Tanzania

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza katika kikao kazi cha Mawaziri na Makatibu Wakuu   kuhusu ugonjwa wa Corona (COVID – 19) nchini kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Machi 23, 2020. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Muktasari:

Leo Jumatatu Machi 23,2020 Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameongoza kikao cha mawaziri na katibu wakuu kujadili masuala mbalimbali kuhusu mikakati ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona (CODIV-19) huku akitangaza kamati tatu alizoziunda za kuhakikisha corona haisambai nchini humo.

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kuhakikisha inazuia ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) isiweze kusambaa kwa kiasi kikubwa nchini humo. 

Pia, waziri mkuu amevishukuru vyombo vya habari nchini Tanzania kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Machi 23, 2020 wakati akizungumza na mawaziri na makatibu wakuu katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma.

Imeelezwa kinga dhidi ya virusi vya corona liwe ni jambo la kimkakati zaidi kuliko kusubiri kutibu, hivyo kwa sasa Serikali imeweka mkazo kwenye kuwahamasisha wananchi kujikinga na virusi hivyo. 

“…mawaziri hakikisheni katika kipindi hiki ziara za kwenda kukagua miradi zielekezwe kwa wakurugenzi ikibidi kwa makatibu wakuu, mawaziri mnatakiwa mjikite katika kukinga Taifa na corona,” amesema Majaliwa 

Wakati huo huo, Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania imeunda kamati tatu kwa ajili ya corona.

Kamati hizo ni ya kitaifa ambayo itaongozwa na waziri mkuu na itahusisha baadhi ya mawaziri, makatibu wakuu na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Kamati ya pili ni ya makatibu wakuu  kutoka sekta husika na itaongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na kamati ya tatu ni ya kikosi kazi cha Taifa ambacho kitaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto huku wajumbe wake wakiwa ni wataalamu akiwamo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema katika kipindi cha saa 24 jumla ya watu 292,142 duniani walibainika kuwa na virusi vya corona kati yao watu 12,784 walifariki.

Pia, katika Bara la Afrika watu 736 walibainika kuwa na virusi vya corona na kati yake watu 20 walifariki katika kipindi cha saa 24.

Akizungumzia kwa upande wa Tanzania, Waziri Ummy amesema jumla ya watu 12 walibainika kuwa na virusi vya corona tangu mgonjwa wa kwanza alivyogundulika nchini Machi 16, 2020 na kwamba wagonjwa wote hali zao ni nzuri na mmoja amepimwa zaidi ya mara mbili na kubainika kuwa hana virusi.