Majaliwa awajibu wanaobeza maagizo aliyoyatoa Zanzibar

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefungua semina ya ushiriki wa vyombo vya ulinzi na usalama katika usimamizi na udhibiti wa rasilimali madini katika ukumbi wa Mtakatifu Gaspar jijini Dodoma huku akizungumzia ziara aliyoifanya hivi karibuni Zanzibar.

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kasim Majaliwa amesema ni haki yake kutoa maagizo katika miradi iliyoko Zanzibar na wanaombeza hawajui majukumu yake.

Waziri Mkuu ameelezea ziara yake hivi karibu alipokuwa Zanzibar alikuta miradi mizuri inayojengwa na serikali ya mapinduzi lakini alipotoa maagizo, watu wakabeza hana mamlaka kwa upande huo wa muungano.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumapili Januari 26,2020 wakati akifunga mafunzo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu ulinzi wa rasilimali madini.

Majaliwa amesema yeye ni mtendaji mkuu wa Serikali ya Tanzania na msimamizi wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye anastahili kueleza mafanikio ya serikali zote katika mkutano mkuu wa chama chake.

"Hivi karibuni nilikuwa Zanzibar ambako nimejionea kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi, lakini nilifika katika miradi fulani nikatoa maagizo, sasa kuna watu wakaanza kuhoji hilo," amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema ataendelea kuhoji na kukosoa au kukemea inapobidi kwa kuwa kazi hiyo ni yake.

Katika hatua nyingine, amekemea ukamataji hovyo wa wawekezaji wa madini akisema unasumbua wawekezaji ambao wameweka mitambo yao mikubwa yenye gharama.

Ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwa makini na hilo kwa kuwa wawekezaji wanalalamika usumbufu huo.

“Katika kipindi cha hivi karibuni kumejitokeza malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji na wadau wa madini kuhusu kukamatwa au kubughudhiwa bila sababu za msingi. Kutokana na hali hiyo, natumia nafasi hii kukemea suala la ukamataji holela wa wawekezaji au wadau wa madini pasipo kufuata taratibu,” amesema

Majaliwa amesema kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama vinatakiwa vitumie Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali iliyowekwa mahsusi kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini. 

 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuviagiza vyombo vya Dola kusimamia na kudhibiti utoroshwaji wa madini na kuhakikisha kuwa masoko yote ya madini  nchini yanalindwa.

“Nyote mtakubaliana nami kwamba kila taasisi ina utaalamu na wataalamu wake. Kwa hivyo, hatuna budi kufanya kazi kwa kuheshimu na kutambua utaalamu ama taaluma za wengine tunaoshirikiana nao.” 

Waziri Mkuu amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ina ofisi mikoa yote ya Tanzania Bara, hivyo hakuna sehemu ambayo wanaweza kusema walikosa msaada wa kitaalamu. “Ni wajibu wetu sote kama watumishi wa umma kujenga mazingira rafiki ya kazi, kuaminiana na kufanya kazi kwa ushirikiano.”