HABARI MPYA: Majaliwa awasimamisha kazi watumishi saba Morogoro

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Jumapili ameendelea na ziara yake mkoani Morogoro ambapo amewasimamisha kazi watumishi saba wa halmashauri za Kilombero na Mji wa Ifaraka wakituhumiwa kwa ubadhirifu.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi saba katika halmashauri mbili za wilaya ya Kilombero na Ifaraka mkoani Morogoro kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha zaidi ya Sh1.3 bilion za makusanyo ya mapato ya ndani.

Mbali na kuwasimamisha kazi watumishi hao, pia Majaliwa ameagiza watumishi hao warejeshe fedha hizo ndani ya siku tatu kabla hajamaliza ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

Pamoja na maagizizo hayo, Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara (DED),  Fransis Ndulane anayedaiwa  Sh5 milioni alizoingiziwa katika akaunti yake bila maelezo yeyote kuzirejesha ndani ya siku tatu.

 

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi hao leo Jumapili, Septemba 15, 2019 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, akiwa katika siku ya pili za ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

“Mkoa mzima wa Morogoro umekuwa na tatizo la upotevu wa mapato, fedha zinakusanywa zinapita mikononi mwa watu hazifiki benki, hii ni shida, hatutavumilia.”

Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) kipindi cha mwaka 2016 hadi Juni 2019, katika mji wa Ifakara  makusanyo yalikuwa ni Sh2.7 bilioni ambapo fedha iliyopelekwa benki ni Sh1.9 bilioni   na kwamba kiasi cha Sh727 milioni hazijulikani zilipoenda. 

Amesema katika mitambo kumi  ya ukusanyaji wa mapato iliokaguliwa imeonyesha kiasi cha Sh348 milioni zilizokusanywa hazikupelekwa benki na hivyo kuishia mikononi mwa watu.

Waziri Mkuu amesema katika uchunguzi huo ilibainika fedha hizo ziliingizwa katika akaunti mbalimbali za watumishi wa halmashauri hizo  kutoka kwa mtendaji wa Kata ya Viwanja 60 katika Mji wa Ifakara aitwaye Gregory Midas.

Watumishi   hao ni  Reina Mrema ambaye anadaiwa kuchukua kiasi cha Sh298 milioni, Haile Njitango Sh73 milioni, Linus Mdembo kiasi cha Sh2 milioni kwa kushirikiana na mtendaji huyo wa Kata.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameagiza Mkuu wa Kitengo cha Tehama katika halmashauri ya Mji wa Ifakara, John Mvanga ambaye ndiye alibaini kuwepo na ubadhilifu wa fedha hizo na badaye kusimamishwa kazi, arejeshwe kazini mara moja na asibughudhiwe.

“Mlimsimamisha kazi  kwa sababu mlijua amegundua madudu yenu, lakini haisaidii, arejeshwe kazini naagiza apewe ulizi  wakutosha.”

Kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero, Waziri Mkuu amesema  zaidi ya Sh600 milioni hazijulikani zilipo huku  kiasi cha Sh98.5 milioni zikidaiwa kuingizwa katika akaunti za watumishi wa halmashauri hiyo bila maelezo yeyote.

Waziri Mkuu amewataja watumishi hao kuwa ni Devid Onyango aliyechukua kiasi cha Sh51 milioni, Elakada Kanongole Sh36 milioni, Fork Karunde Sh8 milioni  na Charlse Chali Sh2.5 milioni.

Amesema kati ya Sh600 milioni kampuni ya Kilombero Plantation LTD (KPL) ambao wanadaiwa kiasi cha Sh531 milioni ambazo hazikuingizwa katika mfumo huo.