VIDEO: Kassim Majaliwa awataka wakurugenzi wawili kuripoti Dar es Salaam

Thursday October 17 2019Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa 

By Irene Bwire, Ofisi ya Waziri Mkuu

Lindi. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama (DED) na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, wafike ofisini kwake Dar es Salaam kesho Ijumaa Oktoba 18, 2019 asubuhi na taarifa kuhusu skimu wa umwagiliaji wa Narunyu.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo mchana Alhamisi, Oktoba 17, 2019 wakati alipoenda kukagua skimu hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa tangu 2017.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama, Warioba Gunze na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, ni Mhandisi Mndeme.

Amechukua uamuzi huo baada ya kufika eneo la mradi na kupokea malalamiko ya wanajumuiya ya umwagiliaji kutoka kwa Mwenyekiti wao, Bw. Bakari Awadhi juu ya kusuasua kwa mradi huo lakini alipotaka apate maelezo ya wataalamu hakuna hata mmoja ambaye alikuwepo.

"Nilitaraji niwakute hapa Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Umwagiliaji wa Wilaya na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda. Nimeagiza wanikute uwanja wa ndege Lindi au Dar es Salaam na kesho asubuhi waje ofisini kwangu wanipe taarifa kamili ya mradi huu. Nataka nijue fedha zilizobakia zaidi ya sh. milioni 240 ziko wapi."

"Walipaswa niwakute hapa wananisubiri kwa sababu nilitoa taarifa tangu jana kwamba nitapita hapa. Nimepata taarifa kwamba wamesafiri kutoka Mtwara na leo asubuhi walikuwepo Lindi mjini. Waje ofisini kesho, wakishindwa, nitachukua maamuzi mengine," amesema.

Advertisement

Akielezea umuhimu wa mradi huo wakati akizungumza na baadhi ya wanaushirika waliokuwepo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ni wa muhimu kwa sababu unatiririsha maji wakati wote. "Huu ni mradi wa kuringia. Mradi huu unatiririsha maji wakati huu wa kiangazi, tena mengi tu."

Amesema kutokana na umuhimu wa mradi huo, hivi sasa wangekuwa wanazalisha mazao ya kila aina.

"Hapa ni mahali pa kuzalisha mazao mengi, leo unalima mahindi, ukivuna unapanda matikiti, ukitoa unapanda nyanya. Sasa nitapasimamia mwenyewe," amesisitiza Waziri Mkuu

Amewataka wanaushirika wanaounda jumuiya ya umwagiliaji wahakikishe kila mmoja anatambua eneo lake na mara kazi ikianza wawe tayari kuanza kilimo.

"Huu mradi una manufaa kwa watu wa Ruo, Mahumbika hadi Mnazi Mmoja. Lazima tuung'ang'anie kwa sababu kuna idadi kubwa ya wakulima wanaoutegemea. Huu mradi lazima tuuvalie njuga," amesema Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofika uwanja wa ndege wa Lindi, maofisa hao walikuwa hawajafika kwa sababu simu zao hazikupatikana, na akaagiza waje Dar es Salaam kesho asubuhi.

Mapema, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika mafaili aliyoyapitia ofisini kwake alibaini kwamba mradi huo ulitengewa Sh788 milioni  ambapo mkandarasi wa kwanza Chest Investments Company alilipwa Sh121 milioni lakini akashindwa kazi.

"Mkandarasi wa pili ambaye ni D & L naye alilipwa zaidi ya shilingi milioni 400 naye pia akashindwa kazi ya kuondoka tope. Kwenye ripoti, inaonesha zilibakia Sh249 milioni," amesema Kassim Majaliwa.

Naye Mwenyekiti wa wanajumuiya ya umwagiliaji ya Narunyu,  Bakari Awadhi alisema skimu hiyo yenye ukubwa hekta 1,200 imekuwa ikijaa maji na kufunika mitaro na hatimaye kujaa mchanga.

Alimwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa awasaidie kuifufua skimu hiyo kwa sababu inawanufaisha wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.

 

 

Advertisement