Majaliwa azungumzia mikopo ya wanafunzi

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imekusanya mikopo iliyoiva ya  Sh183.3 bilioni  sawa na asilimia 116.2 ya lengo la kukusanya Sh157.7 bilioni.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imekusanya mikopo iliyoiva ya  Sh183.3 bilioni  sawa na asilimia 116.2 ya lengo la kukusanya Sh157.7 bilioni.

“Natambua baadhi ya wahitimu wamepata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, natumia  fursa hii kuwakumbusha wote mlionufaika na mkopo wa Serikali katika kutimiza ndoto zenu za kupata elimu ya juu, mkumbuke kurejesha mikopo,” amesema Majaliwa.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo mchana Ijumaa Novemba 29, 2019 wakati akizungumza katika mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), jijini Dar es Salaam.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kila anayenufaika na mkopo asaidie wengine ili nao waweze kufaidika na utaratibu huo wa kukopa na kulipa.

Amebainisha kwamba bila kufanya hivyo Serikali itashindwa kuwajengea uwezo wananchi wake wa kupata fursa zinazojitokeza za elimu katika ngazi mbalimbali.

“Ikumbukwe kuwa maendeleo ya Taifa lolote yanategemea uwekezaji katika rasilimali watu. Nitoe rai kuwa wote mliokopeshwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu mfanye hima kulipa,” alisema Majaliwa

Mtendaji mkuu huyo wa Serikali amewataka amewataka wahadhiri na wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu vilivyopo Dar es Salaam kuchangamkia  fursa ya kupata nyumba na vyumba vya kupangisha katika miradi ya ujenzi wa nyumba za NSSF, NHC na watumishi Housing zilizopo Kigamboni.

Amesema amemuagiza mkurugenzi mkuu wa NSSF kutenga maghorofa watakayoishi wahadhiri na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na vyuo vikuu kuacha kuwatoza kiwango kikubw acha fedha, badala yake wapange bei mpya za kupangisha ambazo wanachuo watazimudu.

Ili kufanikisha utekelezaji  wa jambo hilo, Majaliwa amewashauri viongozi wa taasisi za elimu ya juu za Mkoa wa Dar es Salaam kufanya mawasiliano na taasisi hizo kufikia makubaliano namna ya kupangisha.

Kuhusu kuboresha usafiri wa wanafunzi watakaoishi kwenye nyumba hizo, Majaliwa amesema wameshatoa maelekezo  kwa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwemo wakuu wa Wilaya za Kigamboni na Temeke kukutana na uongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (Latra) kupanga safari za mabasi ya abiria kutoka Tuangoma, Mtoni Kijichi hadi eneo la Feri Kigamboni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango amesema ili IFM kiweze kuwa chachu ya mabadiliko ya uchumi ni lazima uongozi wa chuo hicho kutekeleza sera ya elimu kwa vitendo na kuwa wabunifu kupitia upya mitalaa, ufundishaji na kufanya tafiti.

Wahitimu 2,775 wametunukiwa tuzo mbalimbali na wanafunzi 20 wa shahada ya usimamizi wa fedha wamepongezwa.