Majaliwa kuteta na wanahisa wa CRDB Arusha

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB,Abdulmajid Nsekela(kushoto)akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo,Ally Laay(kulia) baada ya mkutano na waandishi wa habari jijini Arusha leo,katikati ni Mkurugenzi wa idara ya tahadhari za kifedha(Risk and Compliance),Anderson Mlabwa.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzungumza na wanahisa zaidi ya 1,000 wa benki ya CRDB jijini Arusha ambako wanahisa watajadili mipango ya benki

Arusha. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzungumza na wanahisa zaidi ya 1,000 wa benki ya CRDB jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Mei 15, 2019 mkurugenzi mkuu wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema Waziri Mkuu atazungumza na wanahisa wa benki hiyo ijumaa.

"Kwa mara ya kwanza, Waziri Mkuu atafungua semina ya wanahisa wa benki kutoka maeneo mbalimbali nchini siku ya Ijumaa ambapo licha ya kujadili fursa za kiuchumi watajadili mipango ya benki," amesema.

Amesema baada ya ufunguzi huo,wanahisa wa benki hiyo watakuwa na mkutano mkuu ambao utajadili pendekezo la gawio la wanahisa mwaka 2018.

Nsekela amesema wanahisa pia watapokea taarifa za fedha,watachaguwa wajumbe watano wa bodi na kuidhinisha wakaguzi wa hesabu.

"Tunaomba wanahisa kujitokeza kwenye mkutano huu muhimu kujadili maendeleo  ya benki " amesema

Mkurugenzi wa masoko wa CRDB, Tully Mwambapa amesema semina na mkutano mkuu wa benki hiyo ni fursa nzuri ya wanahisa na wateja wa benki hiyo kujua mikakati ya benki na maendeleo  yake.