Majeruhi 16 ajali ya lori Morogoro waendelea kuimarika, waanza mazoezi

Tuesday August 20 2019

 

By Lilian Lucas, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Mganga Mkuu Mkoa wa Morogoro nchini Tanzania, Dk Kusirye Ukio amesema hali ya majeruhi 16 wa ajali ya lori la mafuta waliolazwa Hospitali ya Rufaa mkoa huo wanaendelea vyema.

Majeruhi hao walinusurika katika ajali iliyotokea Jumamosi ya Agosti 10 mwaka 2019 eneo la Msamvu mkoani Morogoro baada ya lori lililokuwa na shehena ya mafuta ya petroli kuanguka kisha kulipuka moto ambapo imesababisha vifo 97 hadi jana Jumatatu na majeruhi 18 waliolazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na 16 Morogoro.

Dk Ukio alisema hayo jana Jumatatu Agosti 19,2019 wakati akipokea msaada wa dawa na vifaa tiba toka Chuo Kikuu Mzumbe wenye thamani ya Sh6.3 milioni ambapo wanafunzi na wanajamii ya chuo hicho walijichangisha kwa ajili ya kusaidia majeruhi hao.

Alisema misaada kama hiyo endelevu ni muhimu kwa hospitali kwani imeendelea kutopea majeruhi wa ajali mbalimbali zinazoendelea kutokea na kwamba msaada huo utalenga katika kuboresha miundombinu ya kuokoa huduma za dharura za kiafya.

Dk Ukio alisema baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo ya lori la mafuta wameanza mazoezi na imani kuwa matibabu yanafanyika vyema na endapo wataendelea na kuimarika wataruhusia pindi madaktari na wauguzi watakapojiridhisha na afya zao.

Akikabidhi msaada huo wa vifaa na dawa, Makamu Mkuu wa  Chuo Kikuu cha Mzumbe Profesa Lughano Kusiluka alisema kama Watanzania tangu kutokea kwa ajali ya moto wamekuwa mstari wa mbele kujitolea katika huduma ikiwa ni pamoja na kuchangia damu ili kuokoa maisha ya majeruhi.

Advertisement

Kwa upande wake, kaimu katibu tawala Morogoro, Noel Kazimoto alisema msaada wa dawa si kwamba utatumika kwa majeruhi pekee wa ajali ya moto, bali zitasaidia kwa wagonjwa wengine ambao wanahitaji msaada wa aina hiyo kutokana na wao kutokuwa na uwezo.

“Hili tatizo la ajali ni kubwa sana si tu kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro bali ni kwa nchi nzima kwa sababu tumepoteza nguvu kazi kubwa ambayo ingeweza kusaidia katika kuleta maendeleo kwanza kama familia na nchi nzima,” alisema Kazimoto.

 

Advertisement