Majeruhi ajali ya Morogoro waruhusiwa, wahamishwa wodi

Morogoro. Hali za majeruhi wa ajali ya lori la mafuta ya petroli kuanguka kisha kuwaka moto mkoani Morogoro zinaendelea vizuri na baadhi yao wameruhusiwa kutoka hospitalini huku wengine wakihamishwa wodi.

Ajali hiyo iliyotokea asubuhi ya Agosti 10 eneo la Msamvu, Morogoro hadi jana vifo vilivyotokana na kadhia hiyo vilikuwa 104 huku majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali mbili tofauti.

Katika Hospitali ya Rufaa Morogoro kulikuwa na majeruhi 18 na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam walikuwa 47 ambapo hadi jana waliokuwa wamebakia ni 11 kati ya 47 na wengine wakifariki.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Morogoro, Dk Ritha Lyamuya akizungumza na Mwananchi jana alisema majeruhi waliobaki kwa sasa ni sita baada ya wanne kuruhusiwa.

Dk Lyamuya alisema majeruhi hao waliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya hali za vidonda vyao kuendelea vyema na kwamba majeruhi sita waliobaki wodini wanaendelea kupatiwa matibabu.

Alisema awali majeruhi nane waliokuwa wamelazwa katika hospitalini hapo waliruhusiwa kwa nyakati tofauti na kubaki majeruhi kumi ambapo kati ya hao wanne wameruhusiwa na kufikia idadi ya majeruhi 12.

"Hapa tangu mwanzo majeruhi waliobaki walikuwa 16, tunachoshukuru hali ya majeruhi waliobaki hawa sita iko vyema na hii nzuri kutokana na juhudi za wauguzi na madaktari wetu pamoja na wananchi kwa namna walivyojitoa," alisema.

Alisema majeruhi hospitalini hapo waliongezeka na kufikia 18 baada ya awali kuwa 16 lakini wawili waliokuwa nyumbani baada ya kutokea kwa ajali kuamua kwenda hospitalini kwa matibabu baada ya hali zao kutokuwa nzuri.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano wa MNH, Sophia Sofia Fabian Mtakasimba alisema hali ya majeruhi 11 inaendelea vizuri baada ya majeruhi mmoja kati ya watano aliyekuwa chumba cha uangalizi maalum (ICU) kuhamishwa.

Alisema awali majeruhi waliokuwa ICU walikuwa watano lakini sasa  wamebaki wanne baada ya mmoja kuhamishiwa wodi namba 22 ya Sewahaji kuungana na wenzake sita kuendelea na matibabu.