OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Majeruhi wa Entebbe mjini Nairobi-14

Muktasari:

  • Katika mfululizo wa makala haya tulizungumzia kilichotokea tangu Juni 27, 1976 ilipotekwa ndege ya Shirika la Ndege la Ufaransa, Flight 139, hadi Julai 4, 1976 mateka walipookolewa mjini Entebbe. Uwanja wa Ndege mjini Nairobi ndio ulikuwa kituo kikuu kati ya Tel Aviv, Israel na Entebbe, Uganda. Endelea…

Gazeti la Kenya, ‘Sunday Nation’ lilichapisha habari za shambulio la Entebbe lililofanyika usiku uliopita. Kuipata habari hiyo mapema kiasi hicho huenda kulitokana na mhariri wake, George Githii, ambaye alikuwa ameondoka Israel saa chache kabla ya shambulio na huenda alikuwa amepata taarifa zozote za kile ambacho kingetokea na kwa hiyo walisubiri hadi kitokee ndipo waende mtamboni.

Jarida la ‘Daily Graphic’ toleo la 8029 la Agosti 12, 1976 liliandika kuwa “Bw George Githii (ambaye pia alikuwa katibu binafsi wa Rais wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta) alikuwa amealikwa Israel wakati mpango wa kuivamia Entebbe ukiandaliwa. Hayo yameandikwa katika ukurasa wa 71 wa jarida hilo. Kwa hiyo habari hiyo ilipochapishwa gazeti hilo lilipanda kwa kasi sana.”

Kwa kuwa Githii alikuwa katibu binafsi wa Mzee Kenyatta, na kwa kuwa alikuwa amealikwa kwenda Israel katika lile juma la utekaji ule, basi inawezekana alijua mambo mengi kuhusu utekaji huo. Huenda hii nayo ikaeleza ni kwa nini zile ndege mbili za Shirika la Ndege la Israel (El Al) zilitangulia Kenya na kupokewa na ulinzi wa polisi. Kama tulivyoeleza katika moja ya matoleo yaliyopita, ndege hizo ziliondoka Israel na kutua Kenya kabla ya ndege za Jeshi la Israel (IDF) kuanza safari ya kwenda Entebbe.

Katika ukurasa wa 122 wa kitabu chake, ‘Hijacking and Hostages: Government Responses to Terrorism’, mwandishi wake, J. Paul de B. Taillon, anasema msaada wa Kenya ulizidi hata kiwango cha usalama wa ndege na kuzijaza mafuta kwa zile zilizofanywa zionekane kuwa ni ndege za abiria zilizoruka kutoka Entebbe. “Kenya, kwa kweli, ilitumika sana katika kuficha ‘mpango wa kuhadaa’ wa Israel.”

Ndege mbili, Boeing 707 yenye namba za usajili LY 167, ilitua mjini Nairobi saa 5:26 usiku ikitokea Entebbe. Ilitua kama ndege ya kiraia lakini ilikuwa ni ya kijeshi na namba zake ni 4XBY8. Ingawa ilitangazwa kwamba imewasili kutoka Tel Aviv, ukweli ni kwamba iliwasili kutoka Entebbe.

Saa mbili baadaye saa 8:06 usiku, ndege ya pili, Harcules, nayo ikatua. Ndege hii ya pili ndiyo ilikuwa imewabeba majeruhi wa shambulio la Entebbe. Majeruhi hao walihamishwa kutoka kwenye Hercules na kuhamishiwa kwenye ndege aina ya Boeing 707 iliyokuwa uwanjani Nairobi tangu jana yake mchana na ambayo ilikuwa na vifaa “muhimu sana” vya tiba.

Wayahudi waliookolewa kutoka Entebbe walishuka kutoka kwenye ndege iliyowafikisha Nairobi na ndipo walipopata mlo pamoja na huduma nyingine muhimu. Hata hivyo, kwa mujibu wa kitabu kilichotajwa hapo juu, ‘Hijacking and Hostages: Government Responses to Terrorism’, wote hao walionywa wasitoe taarifa yoyote kwa yeyote kwa hofu kwamba Kenya wangelipizwa kisasi na wenzao wa Uganda.

Magari ya wagonjwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nairobi (Embakasi)--sasa Jomo Kenyatta yalibeba majeruhi na kuwakimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta ambako wauguzi wa Canada walilazimika kuwaongezea damu.

Muuguzi mmoja raia wa Canada, baada ya kutoa taarifa ya mahitaji ya damu, alishangaa kuwaona wanajeshi wa Israel wakiwasili kwa ajili ya kujitolea damu.

Baadaye muuguzi huyo alisema alishangaa kuona kuwa tayari wanajeshi hao walijua ni kundi gani la damu lilihitajika. Lakini kwa baadhi ilikuwa ni kuchelewa mno. Wakiwa hospitalini hapo, mateka mmoja aliyeokolewa Entebbe, Pasko Cohen, ambaye alihitaji damu kwa haraka, alifariki dunia kabla hakujapambazuka.

Ndege za Israel, baada ya kujaza mafuta, zilianza safari ya kurejea makwao. Ndege ya mwisho ya Hercules iliondoka Nairobi kiasi cha saa mbili kabla hakujapambazuka. Baada ya hiyo Hercules kuondoka, ndipo Boeing 707 iliyotumika kama hospitali ikawa ya mwisho kuondoka, lakini ikiwaacha katika Hospitali ya Kenyatta wanajeshi wawili na mateka mmoja waliokuwa wamejeruhiwa vibaya na ambao walihitaji uangalizi maalumu.

Baadaye gazeti la Daily Nation liliripoti kuwa ushuhuda wa pekee wa shughuli ngumu ya usiku huo ilikuwa ni damu iliyokuwa imetapakaa mahali ambapo ndege za uokoaji zilikuwa zimeegeshwa. Damu ya majeruhi ilitapakaa sana eneo la maegesho ya ndege hizo wakati wakihamishwa kutoka ndege moja kwenda nyingine.

Wakati hayo yakiendelea mjini Nairobi, usiku wa manane mara baada ya mateka kukombolewa, maofisa waandamizi wa Serikali ya Israel, akiwamo kiongozi wa upinzani nchini humo, Menachem Begin, walikuwa wamekutana ofisini kwa Waziri Mkuu wa Israel, Yitzhak Rabin.

Baada ya majadiliano ya muda na kupongezana kwa kilichotendeka Uganda saa chache zilizopita usiku huo, walikubaliana wangekwenda uwanja wa ndege kuwapokea mateka ambao wangewasili Israel baadaye siku hiyo.

Kwa muda wa saa nane, tangu saa 9:00 alfajiri wakati redio ya kijeshi ilipotangaza kwa mara ya kwanza habari za kukombolewa kwa mateka, familia mbalimbali zilipata habari kutoka kwa waliokuwa wamezipata habari hizo.

Familia hizo ziliambiwa zikusanyike kwenye uwanja mmoja wa michezo kusubiri maelekezo zaidi. Walifika kwenye uwanja huo alfajiri. Ndege zilizokuwa zimewabeba mateka hao zililazimika kwanza kwenda eneo la kijeshi kushusha zana za kijeshi ambazo ni siri kubwa kwa Jeshi la Israel, halafu ziwashushe na makomandoo kabla ya kwenda kuwashusha mateka.

Ilipotimu saa 5:00 asubuhi familia za mateka ziliingia kwenye Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion kutoka kwenye uwanja wa michezo.

Kwa upande wa kamanda wa kikosi cha uokozi aliyeuawa mjini Entebbe, Yonathan Netanyahu ambaye alikuwa mtoto wa mwanahistoria wa Kiyahudi, Ben-Zion Netanyahu, aliyekuwa akiishi Marekani na mama yake Netanyahu aliyeitwa Zila, walilazimika kusafiri kutoka Marekani hadi Israel kuupokea mwili wa mtoto wao. Ben-Zion Netanyahu alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Cornell kilichoko Marekani.

Maziko ya Yonathan “Yoni” Netanyahu aliyezaliwa Machi 13, 1946 mjini New York, Marekani yalifanyika Jumanne ya Julai 6, 1976 ikiwa ni siku mbili tangu mateka kuokolewa na yeye kuuawa, yalihudhuriwa na maelfu ya raia wa Israel wakiwamo maofisa wandamizi wa serikali.

Ingawa Yonathan aliongoza kikosi cha kuokoa mateka zaidi ya 100 waliokuwa wameshikiliwa Uganda, yeye mwenyewe hakuweza kujiokoa. Ingawa aliwaokoa mateka hao, yeye mwenyewe aliuawa katika mapigano.

Miongoni mwa mateka 106 waliokuwa wanashikiliwa Uganda, 102 waliokolewa na watatu waliuawa na wengine wapatao 10 walijeruhiwa. Makomandoo watano wa Israel walijeruhiwa.

Kwa mujibu wa kitabu ‘Encyclopædia Britannica,’ watekaji nyara wote pamoja na askari 40 wa Uganda waliuawa. Ndege 11 za kivita za Jeshi la Anga la Uganda zilizotengenezwa Urusi aina ya MiG-17 na MiG-21 ziliteketezwa.

Kwa kuwa Kenya iliisaidia Israel kwa kiasi fulani katika operesheni hiyo kwa kuruhusu ndege kutua na kujaza mafuta mjini Nairobi, Idi Amin aliamua kulipiza kisasi dhidi ya Kenya. Juma moja baadaye, Jumapili ya Julai 11, taarifa zilizopatikana mjini Nairobi zikadai tangu Julai 4 jumla ya Wakenya 245, wakiwamo wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Entebbe, walikuwa wameuawa na askari wa Idi Amin.

Kufikia Ijumaa ya Julai 16 polisi wa Kenya katika mpaka wa Kenya na Uganda walikadiria kuwa idadi ya wakimbizi wa Uganda waliokuwa wameyakimbia majeshi ya Amin na kuingia Kenya walikuwa kiasi cha 3,000.

Hata hivyo, aliyekuwa wa kwanza kulipiziwa kisasi ni Dora Bloch, mateka wa Israel mwenye umri wa miaka 75 ambaye alikuwa Hospitali ya Mulango mjini Kampala wakati mateka wenzake—pamoja na mtoto wake wa kiume, Ilan Hartuv—wakiokolewa na makomandoo wa Israel mjini Entebbe.

Ilikuwaje hadi akawa hospitali wakati wenzake wanaokolewa? Nini hasa kilimfika Dora?

Itaendelea kesho…