Makinikia yawalaza rumande madiwani CCM, Chadema

Muktasari:

  • Madiwani wanne wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamekamatwa na Polisi mkoani Shinyanga nchini Tanzania kwa kile wanachoelezwa kutaka kufanya mkutano unaohusu kujadili manufaa ya mchanga wa madini ya dhahabu ‘makinikia’ watakavyonufaika nao.

Shinyanga. Polisi Mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania linawashikilia madiwani wanne wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani humo kwa madai ya kukiuka maagizo ya Serikali juu ya mchanga wa madini (makinikia) ambao umetolewa na Serikali kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Mchanga huo umetolewa na mgodi wa Almas wa Williamson Diamond uliopo Mwadui Mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania.

Madiwani hao walikamatwa jana Jumamosi Januari 25, 2020 wakati wakijiandaa kufanya kikao na wenyeviti wa vijiji vyote kwenye kata zao. Lengo la kikoa hicho ilikuwa kuzungumza juu ya mchanga huo na manufaa watakayopata wananchi lakini hawakufanikiwa kufanya kikoa hicho.

Madiwani waliokamatwa ni na kata zao kwenye mabano ni; Abdul Ngolomole (Songwa- CCM), Mbalu Kidiga (Maganzo -CCM), Paul Magembe (Mwadui Luhumbo - Chadema) na Sarah Masinga (Viti Maalum- Chadema).

Mwenyekiti wa kijiji cha Songwa, Damas Francis akizungumzia hatua iliyochukuliwa na polisi alisema imewasikitisha kwani wao hawakuwa na nia mbaya bali ni kutaka kupatiwa uelewa kutoka kwa wawakilishi wao wa wananchi ili kuweza kuwafikishia wananchi.

Aliiomba Serikali kuitisha mkutano wa hadhara na kutoa ufafanuzi kwa wananchi juu ya mchanga huo wa madini ili wananchi waweze kupata uelewa watanufaikaje na madini hayo ambayo tangu yaanze kuchimbwa imepita zaidi ya miaka 50 lakini hakuna manufaa kwa wananchi.

“Tulikuja kuzungumzia  manufaa watakayopata wananchi katika mchanga huu wa madini lakini cha kushangaza tumezuiwa na polisi, wakati mchanga huu ukitumiwa vizuri na kuwekewa utaratibu mzuri utasaidia kupunguza matukio ya uhalifu na uvamizi kwenye mgodi wa Mwadui,” alisema Damas.

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Maganzo, Charles Manyenye alionyesha mashaka kuwa huenda makinikia hayo yakawanufaisha wachache kutokana na kuanza kupewa misukosuko ikiwamo viongozi wao kukamatwa na kutaka haki itendeke kwa wananchi wote.

Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga, Joseph Paul alisema madiwani hao wamekamatwa kutokana na kukiuka maagizo ya Serikali ambayo yalitolewa juu ya mchanga wa dhahabu na kuwataka wananchi kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Januari 21, 2020 Rais wa shirikisho la vyama vya wachimbaji wadogo wa madini Tanzania, John Bina kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika alitoa maamuzi yaliyofikiwa kuwa  wachimbaji watapata asilimia 62 badala ya 15 iliyokuwa awali  huku chama cha wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Shinyanga (Shirema) asilimia tano.

Alisema mabadiliko hayo yalimaliza mgogoro uliokuwapo na kufafanua asilimia saba ya Serikali kama mrabaha, asilimia 0.3 ushuru wa huduma na kinachobaki kitagawanywa kwa mtoa huduma ambaye atapata asilimia 25 na mwenye shamba asilimia nane.