Makonda: Nakubali kuonywa na kukaripiwa, Dk Bashiru amjibu

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amehudhuria mkutano wa ndani wa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na kusema anakubali kuelekezwa pale  anapokosea.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amesema anakubali kuonywa, kukaripiwa na kuelekezwa na viongozi wake akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.

Makonda amesema hayo leo Jumapili Septemba 1, 2019 katika mkutano wa Dk Bashiru wa kukagua uhai wa chama na kufunga mitambo katika majimbo ya Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano wa ndani jimbo la Kawe, Makonda amesema katika mkutano uliopita ambao ulifanyika jimbo la Ubungo vipo vyombo vya habari vilivyoandika habari kuhusia na yeye.

"Nataka mnisikilize na mnielewe, ninakubali kuonywa, kukaripiwa na kuelekezwa na viongozi wangu akiwemo Dk Bashiru," amesema Makonda

Amesema mzazi anapoongea na mwanae ni faida kwake na mimi CCM ni mzazi kwangu.

Kwa upande wake, Dk Bashiru amemtaka mkuu huyo wa mkoa kuendelea kuchapa kazi huku akimweleza ukuu wa mkoa ni bora kuliko ubunge.

"Wewe ni mtoto mdogo sana, wapo wanaosema unautaka ubunge wewe jenga mashule ukuu wa mkoa na ubunge kipi bora, mimi ni mwalimu wako nilikufundisha na nitaendelea kukufundisha leo umeongea vizuri," amesema Dk Bashiru

Aidha katika hotuba yake, Dk Bashiru amesema wapo wanaojiuza kuwa amesimika mitambo rasmi katika jimbo la kawe (ambalo linaongozwa na Halima Mdee- Chadema) kwa kuwa Rais John Magufuli na watendaji wake wanafanya kazi kubwa sana.

"Wale walioomba nafasi mwaka 2017 na wanachama wakawaamini wakae na nafasi zao na kujadili wagombea na sio kuwazunguka makundi yalituumiza sana Dar," amesema Dk Bashiru