Makonda: Ukijifungia ndani kisa corona utakufa njaa

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema  baadhi ya wakazi wa mkoa huo watakufa njaa kwa sababu ya kujifungia ndani kwa kigezo cha kuhofia  ugonjwa wa corona.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amesema  baadhi ya wakazi wa mkoa huo watakufa njaa kwa sababu ya kujifungia ndani kwa kigezo cha kuhofia  ugonjwa wa virusi vya corona.

Makonda amesema hayo leo Jumamosi Aprili 4,2020 wakati akizungumza na wanahabari baada ya kumaliza ziara yake ya kukagua ujenzi wa barabara katika wilaya za Ilala na Kinondoni zinazosimamiwa na  Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura)

Amesema hivi sasa hivi kuna  ugonjwa wa ajabu wa watu kutokwenda kazini kuliko ukubwa wa tatizo la virusi vya corona.

“Haingii akili na siwezi kuelewa, sasa hivi imefika hatua wananchi wa Dar es Salaam wamejifungia ndani wakisubiri corona,” amesema Makonda

“Wanashindwa kutoka kwenda kufanya kazi, wanasubiri ugonjwa unaoitwa corona. Ugonjwa wenyewe ni virusi, wataalam wanasema hausambai kwa njia ya hewa, lakini tumeambiwa tukae ndani tujifungie kwa sababu nje kuna corona, tutakufa na njaa.”

Katika maelezo yake, Makonda amesema hivi sasa baadhi ya watu hawaendi kazini, akitolea mfano kuwa jana Ijumaa alitembelea Ilala na kukuta baadhi ya watu wakifunga maduka kwa sababu ya corona akisema huo ni uzembe.

“Huwezi kufunga duka lako linalokupatia kipato, kwa sababu ya corona. Umeambiwa corona ina njia ya kujikinga, kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na kuhakikisha kutokaa karibu na mtu anayekohoa na kupiga chafya na mwenye homa kali,” amesema Makonda.

Amesema ugonjwa wa corona usiwe kigezo cha watu kujifungia ndani, kinachotakiwa ni kufuata utaratibu wa namna ya kujikinga na virusi hivyo ikiwamo kunawa mikono na sabuni kwa maji yanayotiririka.

Amesema jambo  jingine  wataalam walisema corona inaweza kuingia kwa gharama  ya mikono ya mtu hasa wale wanaopenda kupikichapikicha vidole puani  jambo linalochangia kusafirisha ugonjwa huo  kutoka kwenye kikohozi cha mtu, kuingiza kwenye mwili wako.

“Dawa ni kuacha kupikicha, kunawa mikono na kukaa mbali na unachapa kazi. tumeingizwa kwenye hofu ya ajabu ambayo haijawahi kutokea dunia, watu wanajifungia ndani ya nyumba kisa corona mtakufa na njaa. Tokeni mkafanya kazi, tulichozuia ni uzururaji huna jambo la kufanya unaanzisha safari ya kwenda Tegeta au Mbagala,” amesema

 “Sasa nikuulize swali hapo nyumbani hamkai karibu, hamuongei, ulichokuwa unafanya nyumbani huwezi kufanya ofisini? Tokeni mkafanye kazi acheni uvivu. Hatuwezi kujifungia pahala tukisubiri ugonjwa,” amesema Makonda.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuna watu aliowaita wapuuzi wanaosema Serikali inadanganya, idadi imeongezeka “we taahira kwelikweli kwenu kuna mtu amekufa na corona, kuna mtu anaumwa na corona? Hiyo  idadi imetoka wapi, unataka iwe kubwa ufanyaje.”

“Hatuwezi kuishi hivi ndio maana leo (jana), nimekuja kuwafuatilia wakandarasi wamepaki sababu ya corona. We tukulipe fedha, ili barabara ipite, utapaki sababu ya corona haya mvua ikija nyumba za watu zinabomoka na magari yanaharibika, corona ndiyo kitu gani,” alisema