Makonda, wakuu wa wilaya Dar wamsikitisha Sheikh wa mkoa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amewasili majira ya saa saa 6.30 kwenye kongamano la viongozi wa dini.

Muktasari:

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum amewaomba viongozi kuwa wanafika wanapowaalika kwenye masuala yao.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum amesikitishwa na hatua ya viongozi wa mkoa huo kutofika kwenye kongamano maalum kuelekea uchaguzi, uchumi wa viwanda, amani, mahusiano na ustawi wa taifa.

Amesema walimualika Mkuu wa Mkoa Paul Makonda na wakuu wa wilaya katika kongamano hilo lakini hawakuweza kufika.

Akizungumza katika kongamano hilo leo Oktoba 28, 2019, Sheikh Alhad Mussa Salum amemuomba Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi) anayesimamia sekta ya elimu Mwita Waitara kupeleka salamu zake Serikalini kuwa wanapowaalika wawe wanakubali kwa sababu nao wanasaidia katika mambo mbalimbali ikiwamo amani.

“Tunapowaalika kwenye mambo yetu waje, najua angekuja Makamu wa Rais wangekuja,” amesema.

Juhudi za kuwapata wakuu wa wilaya za Dar es Salaam na mkuu wa mkoa zilishindwa kuzaa matunda.

Akijibu suala hilo, Waitara amesema Serikali inawathamini viongozi wa dini na kwamba, kutokuwepo kwa uwakilishi wa serikali ya mkoa na wilaya ataenda kuzungumza na viongozi wake. “Tutawasiliana nao tujue nini kilitokea, Rais Magufuli (John) anawathamini sana,” amesema Waitara.

Waitara ambaye amemuwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi hao katika masuala mbalimbali ikiwamo kuelekea uchumi wa viwanda.