VIDEO: Makonda amuandikia barua Jafo kuhusu mabasi ya mwendokasi

Wednesday April 01 2020
makondea pic

Dar es Salaam. Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam imemuandika barua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Seleman Jafo aangalie uwezekano wa kuyaruhusu mabasi 200 ya mwendokasi yaliyokwama kwenye bandari kavu ya Ubungo.


Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Aprili Mosi, 2020 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati akizungumza na wananchi wa mkoa huo  katika kituo cha daladala cha Makumbusho, kuhusu changamoto za usafiri hasa katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya  corona.
“Suala la mwendokasi halipo chini ya mamlaka yangu, lazima wana Dar es Salaam mfahamu bali lipo chini ya Tamisemi. Hivi tunavyoongea watu wangu wanamaliza kuandika barua.
“Nimemuomba Jafo aingilie kati, ninafahamu yapo mabasi si chini ya 200 ya mwendokasi yameegeshwa  pale Ubungo bandari kavu. Nafahamu kuna mgogoro lakini kwa hali tuliyo nayo sasa hivi, nimemuandikia barua kuyaruhusu magari yale yaingiea kwenye mfumo ili wakazi wa Kimara wasirundikane na kubanana,” amesema Makonda.


Huku akitoa tahadhari ya mara kwa mara kuhusu virusi vya corona  katika mkutano huo, Makonda amesema hatua hiyo itasaidia wakazi wa maeneo ya Ubungo, Kimara na Mbezi kuwahi kazini. 


Mbali na hilo, Makonda amewaomba wamiliki wa majengo, nyumba na vibanda vya biashara kuwapunguzia kodi wapangaji wao akiasema hali ya kiuchumi sio nzuri kutokana uwepo wa ugonjwa wa corona.


Amesema baadhi ya biashara haziendi vizuri, kuna  watu wamepanga nyumba, kwenye ofisi na apartments  na kwamba amejaribu  kuongea na baadhi ya wamiliki wamekubali.
“Nawaomba wamiliki wa nyumba za kupanga, vibanda, majengo, wapunguze kodi  ya asilimia 50 kwa kipindi cha miezi mitatu. Ili kuwawezesha wananchi wamudu hali ya kawaida.
“Ninawaombeni wenye nyumba wote na majengo mkubali, hivi ninavyoongea kuna watu wenye nyumba na majengo wasiopungua 50 wamekubali kushusha nusu ya gharama ili kumwezesha mpangaji apate akiba ya kutunza ndani mwake,” amesema.

Advertisement