Makonda asema wazururaji watapewa kazi ya kufanya

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amesema watu watakaokamatwa kwenye jiji hilo kutokana na uzururaji hawatapelekwa mahabusu ila watapewa kazi za kufanya

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amesema  kuwa watu watakaokamatwa kutokana na kuzurura katika mkoa huo watapewa kazi ya kufanya na si kwenda mahabusu.


Makonda amesema hayo leo Jumatatu Aprili 06, 2020 wakati alipofanya ziara Mlimani City.


Jana Jumapili Makonda akiwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitangaza kuwa kuanzia leo Jumatatu wataanza kuwakamata watu wanaozurura katika mkoa huo.


Baada ya kutoa kauli hiyo ilizua mijadala kuhusu watu hao watakao kamatwa na wapi watapelekwa baada ya kukamatwa.


“Jana nilisema mbele ya waziri tutakamata wazururaji, sasa watu wanajiuliza wazururaji ni wapi, mzururaji ni mtu yoyote yule ambaye hana kazi anaamka asubuhi anaenda feri kupiga stori, anaamka asubuhi anaenda kwenye hoteli hata hanunui chai yeye yupo tu, anategemea kukutana na bahati njiani, hao tunawakamata.”


Amesema baada ya kukamatwa wazururaji hao hawatapelekwa mahabusu bali watapewa kazi za kufanya  


“Wengine wanasema sasa mkiwakamata mnawapeleka wapi? Hatukupeleki mahabusu, kwenye mkoa huu tuna kazi nyingi ambazo tunalipa gharama kubwa kwa kuwalipa watu, tumeona ni vyema hizo kazi wazururaji wazifanye, ili ukiamka asubuhi kama unaenda kuzurura ujue Makonda atakunyakua ukafanye kazi,” amesema
Amesema tayari mkoa huo umeshabainisha kazi ambazo watapewa watu watakaokamatwa kwa uzururaji ikiwemo kufanya usafi wa mazingira.


“Zipo kazi nyingi zaidi ya saba ambazo tumeziainisha moja wapo ni kwenda kusafisha, hatukufungi, unaenda unafanya kazi siku nzima unarudi nyumbani,”


“Tunataka katika kupambana na corona watu kunawa mikono tunataka na jiji letu liwe safi, wito wangu katika hili ni mmoja tu watu tufanye kazi.”