Makonda ataka Idris aende polisi, Kigwangalla kumuwekea dhamana

Muktasari:

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema atamuwekea dhamana mchekeshaji Idris Sultan ikiwa ataripoti polisi na kukamatwa baada ya kutakiwa kufanya hivyo na  mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema atamuwekea dhamana mchekeshaji Idris Sultan ikiwa ataripoti polisi na kukamatwa baada ya kutakiwa kufanya hivyo na  mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Idris ameweka picha yenye sura yake akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa huku akiandika, “kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a–enjoy siku yake ya kuzaliwa kwa amani.”

Baada ya kuweka picha hiyo, Makonda alichangia na kumtaka mchekeshaji huyo kwenda polisi.

“Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako,” amesema Makonda.

Baada ya Makonda kueleza hayo, Dk Kigwangalla aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, “nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi.”

“Mniambie nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake.  Wameonesha upendo.”

Akizungumza na Mwananchi kuhusu Idris kwenda polisi, Makonda amesema, “nimesema kweli aende polisi sina utani na watu wa aina hiyo.”