Makundi yamchukulia Mbowe fomu kuwania uenyekiti Chadema

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Chadema kutangaza ratiba ya uchaguzi wa viongozi ngazi ya Taifa, baadhi ya makundi ndani ya chama hicho yameanza kumchukulia fomu, Freeman Mbowe ili agombee tena uenyekiti wa chama hicho.

Katika Jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam, mkutano mkuu umeamua kumchukulia fomu mwenyekiti huyo, huku vijana sita wakianza mchakato wa kukusanya Sh1 milioni kwa ajili ya fomu hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, mwenyekiti wa jimbo hilo, Patrick Asenga alisema: “Mkutano mkuu uliazimia na tuna kauli mbiu ya ‘Mbowe Tena’. Tumeshawishika kutokana na msimamo na uimara wake kwa kuwa amekipitisha chama katika mazingira magumu.”

Alisema baadhi ya nyumba za Mbowe zimevunjwa, mashamba yake kuharibiwa na pia madiwani na wabunge wamekihama chama hicho, lakini hakutetereka.

“Angekuwa mtu wa kawaida kwa misukosuko aliyopita angekuwa ameshanunulika lakini Mbowe ni jasiri na kwa mazingira ya Serikali iliyopo madarakani, hatujaona mbadala wake licha ya Chadema kuwa na watu wengi sana wenye uwezo wa kuwa wenyeviti,” alisema Asenga.

Katika hatua nyingine, kundi la vijana wa Dar es salaam linaloongozwa na Twaha Mwaipaya kwa kushirikiana na vijana wengine, wamejitolea kumchukulia fomu Mbowe kwa ajili ya kugombea nafasi ya mwenyekiti.

Alisema wanaanza kuchanga fedha kwa kushirikisha vijana nchi nzima kwa ajili ya kupata kiasi hicho cha fedha.

“Wanachama ndio tunaojua magumu Mbowe aliyopitia amekuwa mvumilivu tunaamini yeye ndio atakayetuvusha kwa kipindi kingine cha miaka mitano,” alisema Mwaipaya.

Alisema kwa mazingira yaliyopo ya ukiukwaji wa demokrasia na uvunjwaji wa sheria sio rahisi mtu kuvumilia kuiongoza taasisi hiyo na ikabaki imara.

Naye Mwenyekiti wa baraza la vijana la Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi alisema uamuzi uliochukuliwa na vijana hao si maelekezo ya baraza hilo bali ni utashi wao.

“Kama kuna vijana wanachanga fedha kwa ajili ya kumchukulia mgombea yoyote fomu ni kwa utashi wao ofisi yangu haina taarifa sisi tunafuata misingi ya demokrasia,” alisema Ole Sosopi.

Uchaguzi wa mwenyekiti wa Chadema na viongozi wengine e wa juu unatarajiwa kufanyika Desemba 18, mwaka huu wakati wa mkutano mkuu.