VIDEO: Mambo manane matokeo ya darasa la saba

Muktasari:

Baraza la Taifa la Mitihani nchini Tanzania (Necta) jana Jumanne Oktoba 15, 2019 lilitangaza matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 ambapo asilimia 81.50 ya watahiniwa 933,369 wamefaulu.


Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Mitihani nchini Tanzania (Necta) jana Jumanne Oktoba 15, 2019 lilitangaza matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 ambapo asilimia 81.50 ya watahiniwa 933,369 wamefaulu.

Mwananchi linakuchambulia mambo manane yaliyojitokeza katika matokeo hayo ambayo yanaonyesha ufaulu umeongezeka kwa asilimia 3.78 lakini ufaulu katika somo la Kiingereza bado mdogo likilinganishwa na masomo mengine.

Kiwango cha ufaulu

Kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia 78.38 mwaka 2018 hadi asilimia 81.50. Ongezeko hilo ni la asilimia 3.78 ambapo jumla ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo ni 933,369.

Wafutiwa matokeo

Wanafunzi 909 waliofanya mtihani huo wamefutiwa matokeo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo udanganyifu. Mwaka 2018 Necta iliwafutia matokeo wanafunzi 357 huku ikitangaza kufuta matokeo ya shule zote za halmashauri ya Chemba na Kondoa mkoani Dodoma.

Mikoa Kanda ya Ziwa yang’ara

Kanda ya Ziwa imeongoza kwa kutoa shule kumi bora kitaifa huku shule ya Graiyaki iliyopo wilayani Serengeti ikibeba bendera ya ufaulu katika kanda hiyo. Mwaka 2018  kanda ya ziwa ilitoa shule nane katika shule 10 bora kitaifa.

Dar na ufaulu

Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa kupata ufaulu wa asilimia 93.28 ukifuatiwa na Mkoa wa Arusha kisha Iringa, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Mbeya, Simiyu, Njombe na Pwani. Hata hivyo, kwa ngazi ya halmashauri Jiji la Arusha limeongoza likifuatiwa na Kinondoni.

Ufaulu Hesabu, Kiingereza washuka

Ufaulu wa masomo ya Hesabu na Kiingereza umeshuka kwa asilimia 1.05 ikilinganishwa na mwaka 2018. Mwaka 2019 watahiniwa wameonekana kufaulu zaidi katika somo la Kiswahili kama ilivyokuwa mwaka 2018 ambapo ufaulu wake ni asilimia 87.25.

Shule 10 zilizofanya vizuri

Shule 10 zilizofanya vizuri kitaifa ni Graiyaki (Mara), Twibhoki (Mara), Kemebos (Kagera), Little Treasures (Shinyanga), Musabe (Mwanza), Tulele (Mwanza), Kwema Morden (Shinyanga), Peaceland (Mwanza), Mugini (Mwanza) na Rocken Hill (Shinyanga).

Wanafunzi 10 bora wavulana

Wanafunzi 10 wavulana na shule kwenye mabano ni Francis Gwai (Paradise), Victor Godfrey (Graiyaki), Aziz Yassin (Graiyaki), Goldie Hhayuma (Graiyaki), Daniel Ngassa Daniel (Little Treasures), Hilary Nassor (Peaceland), Mbelele Dalali (Kwema Modern), Derick Lema (Musabe), Athanas Sekuro (Paradise) na Aron Mabuga (Kwema Modern).

Wanafunzi 10 bora wasichana

Kwa upande wa wasichana wanafunzi 10 bora ni Grace Manga (Graiyaki), Loi Kitundu (Mbezi), Nyanswi Richard (Graiyaki), Neema Mushi (Graiyaki), Maryleocadia Nkuba (Peaceland), Heavenlight Hhayuma (Twibhoki), Roseleader Steven (Twibhoki), Pilly Zacharia (God’s Bridge), Scholastica Shelembi (Little Treasures) na Suzan Fridoline (Little Treasures).