Mambo matano mvua iliyoleta majanga Dar

Muktasari:

Mvua hiyo iliyoanza kunyesha kuanzia saa 2 asubuhi hadi jioni na kusababisha mito kujaa maji yaliyoanza kupita juu ya barabara ilizua sintofahamu kuanzia saa 10 jioni na kusababisha foleni kubwa iliyokuwa chanzo cha wananchi, wakiwemo wanafunzi kufika majumbani usiku wa maanani na wengine kukesha njiani hadi jana asubuhi.

Dar es Salaam. Unaweza kusema mambo makubwa matano ndio chanzo cha shughuli katika Jiji la Dar es Salaam kusimama kuanzia juzi asubuhi hadi jioni baada ya mvua kubwa kunyesha kwa zaidi ya saa 10.

Mvua hiyo iliyoanza kunyesha kuanzia saa 2 asubuhi hadi jioni na kusababisha mito kujaa maji yaliyoanza kupita juu ya barabara ilizua sintofahamu kuanzia saa 10 jioni na kusababisha foleni kubwa iliyokuwa chanzo cha wananchi, wakiwemo wanafunzi kufika majumbani usiku wa maanani na wengine kukesha njiani hadi jana asubuhi.

Sababu hizo ni ujenzi wa baadhi ya barabara za jiji hilo unaoendelea, kutokuwepo kwa askari wa usalama barabarani katika maeneo yaliyokuwa na changamoto, maelekezo yasiyojitosheleza kuhusu barabara zipi zinapitika na zilizofungwa, baadhi ya barabara kutopitika kutokana na kujaa maji na madereva kuchepuka ili kuwahi na kujikuta wakifunga barabara.

Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi jana kuhusu hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge aliahidi kutoa ufafanuzi wa kina juu ya sababu na suluhisho la changamoto sugu ya mafuriko na foleni katika jiji hilo.

“Leo (jana) ndio kwanza nimeanza kukusanya taarifa, naomba unipe muda lakini kesho (leo) nitawaita kwenye mkutano wa waandishi wa habari kueleza mikakati yote tuliyonayo,” alisema Kunenge.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale aliomba atafutwe wakati mwingine kwa lengo la kuzungumzia hatua za kuondoa kero ya foleni kupitia uwekezaji wa miundombinu inayoendelea ndani ya jiji hilo chini ya wakala huo.

Pamoja na changamoto mvua hizo ziligeuka neema kwa madereva bodaboda kutokana na kupata abiria wengi huku ikigeuka kilio kwa daladala na bajaj, kama ilivyokuwa kwa wafanyabiashara wengine wakiwemo mama lishe.

Baadhi ya maeneo katika barabara ya Mandela, Morogoro, Bagamoyo, Nyerere na Kawawa yalikuwa hayapitiki kutokana na barabara hizo kujaa maji, na mamlaka husika kulazimika kuzifunga kwa muda.

Mathalani barabara ya Kawawa eneo la Kigogo, muda wa jioni maji yalikuwa yanapita juu kama ilivyokuwa kwa barabara ya Morogoro eneo la Jangwani na Mandela eneo la Matumbi ambayo yalifungwa kwa muda.

Akizungumza na gazeti hili, Msemaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), William Gatambi alisema huduma ya mabasi hayo yanayofanya safari zake kati Kimara na Morocco pamoja na Kariakoo-Morocco zilirejea juzi saa nne usiku baada ya maji kupungua katika mto Ng’ombe eneo ya Mkwajuni.

Katika barabara ya Morogoro eneo la Jangwani huduma za mabasi hayo zilirejea jana saa 5:30 asubuhi baada ya kuondolewa takataka zilizokuwa zimekwama katika daraja la Jangwani na kusababisha maji kufurika.

Ujenzi unaoendelea katika baadhi ya barabara ikiwemo ya Sinza pamoja na makutano ya Sam Nujoma, Mandela na Morogoro eneo la Ubungo ulisababisha foleni kwa kuwa idadi ya magari ilikuwa ikiongezeka.

Jambo jingine, kutokuwepo kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani katika maeneo yaliyokuwa na changamoto kama hizo kumeelezwa ni oja ya sababu ya madereva kufanya watakavyo na kusababisha magari kufungana.

Hali hiyo ilisababisha foleni ya magari kuanzia Ubungo hadi Tazara, eneo la Mwenge kuelekea katikati ya jiji kupitia barabara ya Bagamoyo kutopitika kwa zaidi ya saa tano na kusababisha watu kushuka kwenye daladala na kutembea kwa miguu, wengine wakiegesha magari yao au kuyazima wakiwa kwenye foleni.

“Nimefika nyumbani saa 9:00 usiku kwa sababu magari yalikuwa hayatembei kutokana na foleni. Ninapofanya kazi na ninapoishi ni umbali kwa kilomita 11 tu nilitumia saa 8 kutoka kazini hadi nyumbani,” alisema Cyprian Kaijage.

Kulikuwa na changamoto ya kuelekeza watumiaji wa barabara maeneo gani wapite hali iliyosababisha wenye magari kupita barabara ambazo zilikuwa na changamoto ya foleni.

“Nilitumia saa tatu kutoka Buguruni mpaka Kariakoo, kwa kuwa nilikamilisha jambo langu nilianza kurudi Mbezi ambapo nilitumia njia ya Buguruni ili nipite Tabata kwa kuwa nilisikia mitandaoni kuwa kuna nafuu, ila kilichonikuta nilikaa barabara ya Uhuru kuanzia saa 11 jioni mpaka saa 9 usiku ndipo nilifanikiwa kufika Tabata na kisha kuelekea Mbezi,” alisema Omary Ally.

Katika baadhi ya barabara kutokana na changamoto ya foleni, magari yalikuwa yakiovateki kwa lengo la kuwahi mbele hali iliyosababisha yafungane, hivyo kuyazuia hadi yaliyokuwa yanatakiwa kupita upande wa pili wa barabara husika.

“Hali hii ilikuwa zaidi pale Tabata mataa, Mwenge kuelekea katikati ya jiji na hata Tazara kwenda uwanja wa Uwanja wa Ndege. Pia barabara za mitaani nazo hazikuwa zikipitika maana magari yalifungana. Kuna ile barabara ya jeshini kutokea Makoka, Segerea mwisho na Kisukuru nayo ilifunga hivyo hivyo, “ alisema Cleophas Morris, dereva bodaboda eneo la Ubungo.

Mbali na changamoto hizo, Mwananchi jana lilitembelea maeneo mbalimbali na kuzungumza na watu wa kada mbalimbali huku waandishi wakishuhudia mwili wa mtu uliodaiwa kuokotwa katika mto Msimbazi.

Yaacha vilio, vicheko

Athari za moja kwa moja zimeonekana kwa wafanyabiashara wa maduka, mama ntilie, wachuuzi wa bidhaa, madereva wa daladala, bodaboda, wafanyakazi, wanafunzi.

Mwananchi imetembelea maeneo mbalimbali jana na kushuhudia uharibifu uliotokea baada ya mvua hiyo kunyesha mfululizo, huku baadhi ya wafanyabiashara wakielezea athari walizozipata.

Fadhili Joseph, dereva daladala anayefanya safari zake kati ya Gongo la Mboto na Masaki, alisema alipata hasara lakini licha ya kuwa hesabu ya siku husika haikupatikana, alilala barabarani na akatumia fedha nyingi kujaza mafuta.

“Kwa kawaida ninafanya safari sita kwa 12 , lakini jana nilifanya tatu na nusu, hasara niliyoipata ni ya mafuta na makusanyo. Kawaida kwa siku nakusanya Sh490,000 jana nilipata Sh240,000 kwa ile foleni ya jioni nilitoka Gongo la Mboto saa nane mchana nilifika Masaki saa 6 usiku,” Alisema Fadhili ambaye hutumia Sh60,000 kwa siku kuweka mafuta lakini juzi alitumia Sh110,000.

Aidha Nassor aliiomba serikali itanue barabara iongeze mifereji maji yatembee yasizibe barabara.

Selemani Sebegere ambaye ni dereva bodaboda alieleza jinsi alivyopata faida kutokana na kupakia abiria wengi waliokuwa wakikwepa kukaa muda mrefu kwenye foleni na hivyo kupata Sh110,000 wakati huwa anapata Sh30,000 hadi 40,000 kwa siku.

Kutokana na mvua ya juzi kuwa kubwa wafanyabiashara wengi walishindwa kufungua biashara zao katika maeneo mbalimbali ndani ya jiji.

Tofauti na siku za kawaida hata soko kuu la Kariakoo nalo maduka mengi yalifungwa kutokanana na mvua.

“Hali ilikuwa mbaya biashara jana (juzi) kulikuwa hakuna biashara, wateja hakuna kabisa, ile mvua haikuwa ya kawaida hata mauzo jana kulikuwa hakuna,” alisema Neema John mfanyabiashara Kariakoo

Michael Mnego mfanyabiashara ndogondogo alisema, “unasimamaje kwa mvua ile zaidi ya kukaa tu hata wenye maduka wengi hawakufungua.”

Catherine Mapunda ambaye ni mama ntilie katika eneo la Masaki mwisho alisema hali ya biashara ilikuwa mbaya kwani wateja wengi waliokuwa wakishuka katika magari walikuwa wakipanda bajaji na kuondoka.

“Mvua ilikuwa kubwa hata sehemu tuliyoweka vitu kwa ajili ya biashara kulijaa maji, vyakula vilibaki hakuna walaji ikiwemo supu, mihogo, vutafunwa na tulipoona hali inazidi kuwa mbaya hatukupika mchana. Hasara ya vyakula hivi inaweza kufika Sh45,000 ambayo siwezi kuirudisha kwa sababu vyakula siwezi kuuza vilivyolala,” alisema.

Mfanyabiashara mwingine, Sophia Mohammed jana alilazimika kuanza kujenga upya banda lake baada ya alilokuwa akitumia awali kuharibiwa na mvua.

“Mbali na kuharibika banda, vitafunwa ninavyopika kwa ajili ya chai yaani mihogo na vutumbua sikuuza hata shilingi moja, ilikuwa ni hasara tupu na hata mtaji wake umepotea. Hapa nalazimika kutumia Sh25,000 kujenga upya banda langu la biashara na mihogo na vitumbua mtaji wake ni Sh18,000 vyote vimepotea,” alisema Sophia.

Jana eneo la Kigogo Msimbazi kijiko kilikuwa kikiondoa uchafu kwenye mifereji ili maji yaliyojaa kwenye nyumba za watu yatoke kuelekea mto Msimbazi.

Makazi wa eneo la Kigogo Msimbazi, Sakina Salehe alisema wanatoa maji na tope yaliyojaa kwenye nyumba take na wakimaliza wanaingiza vitu vyao ndani ili maisha yaendelee

“Mafuriko ya juzi(Jana) hayajawahi kutokea mara nyingi mvua zinaponyesha maji yanaishia kwenye ngazi ya nne lakini haya ya safari hii maji yamepita kwenye madirisha yanaonekana mabati Tu,”alisema Salina.

Makazi mwingine wa eneo hilo, Hilda Mwasege alisema hajaokoa hata kitu kimoja vitu vyake vyote vimeingia maji na tope.