Mambo mazito mchakato wa kumng’oa Trump

Washington.  Wanadiplomasia wawili wa Marekani wametoa ushahidi mzito, yakiwamo madai mapya kuhusu juhudi za Rais Donald Trump kuitaka Ukraine kumchunguza mshindani wake katika uchaguzi wa 2020, Joe Biden.

Ushahidi huo umetolewa na kurushwa moja kwa moja kupitia televisheni, kuanzia jana Jumatano katika kamati ya Bunge inayoendesha uchunguzi wa dhidi ya Trump.

Rais Trump amepuuza uchunguzi huo unaosimamiwa na Bunge linaoongozwa na Chama cha Democrats kuwa ni “kutafuta mchawi” na kuwa ana kazi nyingi hawezi hata kufuatilia mahojiano hayo ambako ameungwa mkono na wabunge wa chama cha Republican.

William Taylor, ofisa wa juu wa Ubalozi wa Marekani nchini Ukraine, alianza kutoa ushahidi wake mbele ya Kamati ya uchunguzi akieleza masuala mapya kuhusu juhudi za Trump kushinikiza Ukraine, hoja ambayo ndiyo msingi wa mchakato huo wanne wa kutaka kumng’oa rais katika historia ya Marekani.

Chama cha Democrats kinamtuhumu Trump kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa kutumia msaada wa kijeshi na Ikulu ya White House kumshinikiza Rais Volodymyr Zelensky kufungua upelelezi dhidi ya Biden na mwanaye Hunter.

Kijana huyo wa Biden alifanya kazi katika bodi ya kampuni moja ya gesi nchini Ukraine iitwayo Burisma.

Ushahidi muhimu ni maelezo ya simu ya ikulu ya Julai 25 kati ya Trump na Zelensky ambapo Tunp anamtaka mwenzake wa Ukraine amchunguze Biden.

Taylor ameileza kamati hiyo kuwa Trump alikuwa anajali zaidi uchunguzi (dhidi ya Buden) kuliko alivyokuwa anaijali Ukraine.

Mwanajeshi huyo wa zamani na mwanadiplomasia mkongwe, ambaye alitoa ushahidi wa siri mwezi uliopita, kuwa alifahamu kuhusu mawasiliano ya simu hiyo kati Trump na Balozi wa Marekani katika Umoja wa Ulaya, Gordon Sondland ambayo mmoja wa wafanyakazi katika ofisi yake alisikia.

Mfanyakazi huyo alimuuliza Sondland baada ya simu kuhusu nini Trump alikuwa anafikiria kuhusu Ukraine na kuambiwa kuwa “alikuwa anajali kumchunguza Biden na mwanaye,” alisema Taylor.