VIDEO: Mambo yameanza uchaguzi Chadema

Muktasari:

Wanachama na makada wa Chadema wameanza kumiminika katika ukumbi wa Mlimani City katika uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.


Dar es Salaam. Wanachama na makada wa Chadema wameanza kumiminika katika ukumbi wa Mlimani City katika uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Katika uchaguzi huo, wajumbe zaidi ya 1,000 watachagua mwenyekiti wa chama hicho na makamu mwenyekiti wa Bara na Zanzibar.

Nje ya ukumbi huo wajumbe wa mkutano huo wamesimama katika vikundi wakijadiliana masuala mbalimbali jambo linalosababisha msongamano wa magari yanayoingia eneo hilo.

Wakati vikundi mbalimbali vikipiga nyimbo za hamasa za chama hicho, ndani na nje ya ukumbi  ulinzi umeimarishwa.

Wajumbe wote wanaoingia ukumbini wanaonyesha vitambulisho vyao mlangoni.

Viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa pamoja na mabalozi ni kati ya wageni walioalikwa na baadhi wameanza kuwasili.

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anawania tena nafasi hiyo na safari hii anachuana na mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe.

Wanaowania makamu mwenyekiti ni aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyepo nchini Ubelgiji, Lissu ambaye ataomba kura kwa njia ya mtandao wa Skype.

Lissu anachuana na mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda.