Mamia wajitokeza Arusha kumzika rubani mwanafunzi

Muktasari:

  • Nelson  Olotu aliyefariki katika ajali ya ndege Jumatatu ya Septemba 23, 2019 amezikwa leo Ijumaa Septemba 27, 2019 kijijini kwao Kwa Mrefu mkoani Arusha. Nelson alizaliwa Novemba 26, 1994.

Arusha. Safari ya mwisho duniani ya rubani mwanafunzi, Nelson  Olotu (24) imehitimishwa leo Ijumaa Septemba 27, 2019 kijijini kwao eneo la Kwa Mrefu mkoani Arusha nchini Tanzania.

Nelson aliyezaliwa Novemba 26, 1994 amezikwa kijijini hapo na mamia ya wakazi wa ndani na nje ya Arusha wakiongozwa na mkuu wa mkoa huo, Mrisho Gambo.

Nelson alifikwa na mauti asubuhi ya Jumatatu Septemba 23, 2019 akiwa na mwenzake, Nelson Mabeyo aliyekuwa rubani wa ndege ya Kampuni ya Auric ambayo ilianguka katika uwanja mdogo wa ndege wa Soronera uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania.

Vijana hao ambao walikuwa wakifanana majina walipoteza maisha papo hapo. Nelson Mabeyo yeye alizikwa jana Alhamisi Septemba 26, 2019 kijijini kwako Masanza wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu.

Ibada ya mazishi ya Nelson Olotu imefanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa  Sasi, iliongozwa na Askofu  Dayosisi hiyo, Dk Solomoni Masangwa.

Akizungumza katika shughuli hiyo ya mazishi, Gambo amesema marehemu ameondoka wakati taifa likiwa linamhitaji kutoka na msukumo wa Serikali kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

"Marehemu Nelson ameacha pengo kubwa kwa familia na Serikali kwa ujumla hasa wakati huu uwekezaji mkubwa ukiwekwa kwenye usafiri wa anga ambapo nguvu kazi ya wataalamu inahitajika sana," amesema Gambo aliyekuwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro, Mkuu wilaya ya Hai, mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya

Naye Mwakilishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) nchini Tanzania, Herman Mbatio amesema shirika hilo limesikitishwa na tukio hilo la kupoteza maisha kwa vijana hao ambao walikua kwenye jukumu muhimu la kuendeleza sekta ya utalii nchini humo.