Mamia wajitokeza kuipokea Bombardier

Wananchi waliojitokeza katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza ambapo ndege aina ya Bombadier Q 400 itatua kwa mara ya kwanza katika uwanja huo Dec 14. Picha na Johari Shani

Muktasari:

Wananchi na viongozi mbalimbali wameanza kuwasili katika uwanja wa ndege mjini Mwanza kuipokea ndege aina ya Bombardier Q 400 inayotokea Canada ilikokuwa imeshikiliwa kwa siku kadhaa

Mwanza. Wananchi na viongozi mbalimbali wameanza kuwasili katika uwanja wa ndege mjini Mwanza kuipokea ndege aina ya Bombardier Q 400 inayotokea Canada ilikokuwa imeshikiliwa kwa siku kadhaa.

Ndege hiyo inatarajiwa kutua katika uwanja huo leo Jumamosi Desemba 14, 2019 saa 11 jioni.

Rais wa Tanzania, John Magufuli atawaongoza wananchi katika mapokezi hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema, “ kuanzia saa sita mchana hadi saa tisa alasiri watawasili wananchi na viongozi mashuhuri. Rais ataingia uwanjani hapa saa 10:00 jioni na ndege hiyo inategemewa kuwasili saa 11:00  jioni.”

Novemba 23, 2019 katika hafla ya kuapishwa kwa mabalozi mjini Dodoma Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi alieleza kukamatwa kwa ndege hiyo nchini Canada.

Msomi huyo alisema aliyesababisha Bombardier kukamatwa ni Hermanus Steyn, raia wa Afrika Kusini ambaye alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini akidai fidia ya dola 33 milioni.

Kesi hiyo ilisababisha Mahakama hiyo kuizuia ndege ya Tanzania aina ya  Airbus A220-300 kuondoka nchini humo Agosti, 2019.

Steyn, anadai fidia baada ya mali zake kutaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980. Hata hivyo, Septemba 3, 2019 mahakama hiyo iliamuru ndege hiyo iliyokuwa imezuiwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo kuachiwa baada ya Serikali kushinda kesi bila kutoa fedha yoyote.

Baada ya kutangazwa kushikiliwa kwa Bombardier hiyo ambayo imeruhusiwa kuondoka Canada kulirejesha kumbukumbu ya ndege nyingine ya Tanzania aina ya Bombardier Q400-8 iliyozuiwa nchini Canada mwaka 2017 kutokana na madai ya Sh87.3 bilioni zilizokuwa zikidaiwa na kampuni ya kikandarasi.