Mamia wamlilia baba Kanumba, kuzikwa kesho

Muktasari:

Majonzi na simanzi vilitawala katika ibada ya mazishi ya  Charles Kanumba ambaye ni baba mzazi wa aliyekuwa mwigizaji maarufu wa filamu nchini Tanzania, Steven Kanumba.

Shinyanga.  Majonzi na simanzi vilitawala katika ibada ya mazishi ya  Charles Kanumba ambaye ni baba mzazi wa aliyekuwa mwigizaji maarufu wa filamu nchini Tanzania, Steven Kanumba.

Ibada hiyo imefanyika leo jioni Jumanne Februari 10, 2020 nyumbani kwake mtaa wa Magadula kata ya Ngokolo na kuongozwa na mchungaji wa Kanisa la AIC, Zabron Mangwengula aliyewataka waombolezaji kutenda mema.

Zabron amesema maisha ya Charles yalikuwa mikononi mwa Mungu kwa kuwa  binadamu wanaishi kwa uwezo wake, “hakuna anayejua siku wala saa. Binadamu anapaswa kujiandaa muda wote kwa kusali na kufuata mafundisho ya Mungu.”

“Tunapokuwa hai tuna faida mbele ya jamii inayotuzunguka na ndio maana leo hii watu wanalia kwa uchungu kutokana na upendo mkubwa alikuwa akiuonyesha mzee wetu  ambaye leo tunamuaga na kwenda kumpumzisha  kwenye nyumba yake ya milele,” amesema.

Akisoma wasifu wa Charles, Reuben Zakayo amesema alizaliwa mwaka 1949 Kwimba mkoani Mwanza na ana watoto tisa lakini wawili wa kiume wameshafariki dunia.

Amesema alikuwa akisumbuliwa na nyonga na Machi 7, 2020 alizidiwa na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga lakini alifariki dunia siku iliyofuata.

Amewahi kufanya kazi ofisi ya mkuu wa Mkoa Shinyanga idara ya utamaduni, amewahi kuwa ofisa mtendaji wa kata ya Mwawaza, Kambarage, Ndala na hadi anastaafu mwaka 2015 alikuwa kata ya Chamaguha.

Mwenyekiti wa mtaa wa Magadula, Hamphrey Mtafungwa amesema wamepoteza kiongozi aliyekuwa mshauri katika jamii iliyomzunguka.

Maziko yatafanyika kesho Jumatano Machi 11, 2020 katika kijiji cha Nyakaboja Nasa wilaya ya Busega mkoani Simiyu.

Steven Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012.