Maombi ya wadau kwa Serikali ya Tanzania kuhusu ubunifu haya hapa

Tuesday October 22 2019

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]@.co.tz

Dar es Salaam. Wadau wa sayansi na ubunifu nchini Tanzania wameiomba Serikali kuboresha sera ya utafiti ili kuinua ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Oktoba 22, 2019 na Beatrina Diyammet, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia tafiti za sera, kubainisha kuwa sera madhubuti zitasaidia kujua changamoto mbalimbali za ubunifu.

Beatrina ameeleza hayo katika mkutano ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Sera nzuri katika utafiti zitatuwezesha kujua tupo wapi katika ubunifu na tunaelekea wapi, hapa nchini tunaona kila mwaka watu wanabuni lakini kutokana na kutokuwa na sera hatujui mwisho wake,” amesema.

Amesema ubunifu si tu kwa ajili ya kuzalisha ajira,  bali ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote duniani.

“Ukiangalia viwanda vingi nchini vinashindwa kuendelea kwa kukosa ubunifu lakini viwanda vya wenzetu vinaendelea. Hatuwezi kuzalisha bidhaa bora bila kuupa ubunifu kipaumbele.”

Advertisement

“Lengo letu ni kuwajengea uwezo watafiti wetu ili waweze kuandaa kazi za ubunifu zinazochochea maendeleo na si kwa ajili ya maonyesho pekee,” amesema.

Awali, mkurugenzi mkuu wa Costech,  Amos Nungu amesema mkutano huo uliowakutanisha wadau mbalimbali wa sayansi na ubunifu kutoka nchi zinazoendelea Afrika utaleta matokeo mazuri.

“Tutakusanya mapendekezo yatakayotolewa na wabunifu lengo ni kuona kazi za ubunifu zinazovumbuliwa na teknolojia zinakuwa chachu ya maendeleo ya viwanda vyetu,” amesema.

Mkurugenzi mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC),  Profesa Damian Gabagambi amesema sera ya uchumi wa viwanda iendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

“Tunaona teknolojia zinakuwa kila siku, idadi ya watu nayo inaongezeka, ni vyema kasi yetu ya uzalishaji iendane na mabadiliko haya kwa sababu ukiangalia baadhi ya maeneo mambo ni yaleyale ya zamani,” amesema Profesa Gabagambi.

 

Advertisement