Maonyesho ya Uwandae Expo2020 kufanyika Tanzania, nchi saba kushiriki

Friday January 17 2020

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla anatarajia kufungua maonyesho ya siku tatu ya utalii wa ndani yanayotarajia kuanza Februari 6 hadi 8, 2020 katika viwanja vya Jumba la Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam.

Maonyesho hayo yaliyopewa jina la Uwandae Expo2020, yameandaliwa na Chama cha Wanawake katika Tasnia ya Utalii Tanzania (AWOTTA) huku washiriki zaidi 80, zikiwamo nchi saba wakitarajia kushiriki maonyesho hayo.

Wengine watakao shiriki maonyesho hayo ni Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake; mbuga za baharini (Marine Parks) Nyama choma Festival, Dar es Salaam Zoo (Wanyama hai).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 17, 2020, Mwenyekiti wa AWOTTA, Mary Kalikawe amesema lengo la kufanya maonyesho hayo ni kukuza uelewa kwa jamii kuwa utalii wa ndani ni chanzo kikubwa cha ajira kwa Watanzania lakini utalii huo huvutia watalii wengi kutoka nje ya nchi kuja Tanzania kufanya utalii .

 “Kupitia maonyesho hayo, tunataka kutambulisha kuna aina mbalimbali za utalii wa ndani kama utalii wa historia, matibabu, utalii wa mikutano, utalii wa kidini, kiutamaduni, michezo, utalii wa sherehe za kitaifa, utalii wa mitindo, matamasha, utalii wa wanyamapori, utalii wa fukwe na sherehe za harusi,” amesema Mary

“OWATTA tunafanya kazi kwa karibu na Bodi ya Utalii Tanzania na kupitia kazi zetu tunazofanya, tumeteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa chama cha mfano katika bara la Afrika na hii ni kutokana na kuvutia watalii kutoka nje ya nchi kuja nchini kushiriki maonyesho mbalimbali ya utalii,” amesema mwenyekiti huyo.

Advertisement

Mary amesema mpaka sasa kiasi cha dola za Kimarekani 80,000 kimetumika katika maandalizi ya maonyesho hayo yatakayohusisha pia washiriki kutoka mikoa tisa ambayo ni Dodoma, Kagera, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Morogoro, Pwani na wenyeji Dar es Salaam.

Amesema UwandaeExpo 2020 ni maonyesho ya pili kufanyika Tanzania kwani Februari 15 hadi 19, 2019 AWOTTA walifanya maonyesho kama hayo.

Ametaja nchi zitakazoshiriki maonyesho hayo ni Ethiopia, Malawi, Afrika Kusini, Kenya, Angola, Zimbabwe, Ivory Coast, Bodi ya Utalii Afrika na wageni kutoka Umoja wa Mataifa.

Kwa upande, Ofisa Uhusiano Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB), Geofrey Tengeneza amesema mbali na maonyesho hayo kutakuwa na kongamano litakalojadili fursa zilizopo katika utalii wa ndani.

“Natoa wito kwa taasisi mbalimbali kuunga mkono na kushiriki katika maonyesho haya ili tuweze kusonga mbele katika kuuza pato la taifa kupitia utalii wa ndani,” amesema Tengeneza.

Advertisement