Mapito ya Rugemalira, Sethi mwaka mmoja mahabusu

Wafanyabiashara Harbinder Sethi (mwenye kilemba na James Rugemalira katika picha tofauti wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Picha ya Maktaba.

Wafanyabiashara wawili maarufu nchini, Harbinder Sethi na James Rugemalira wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, wakituhumiwa kujipatia fedha isivyo halali kutoka kwenye Akaunti maalumu ya Tegeta Escrow, wamekuwa mahabusu kwa mwaka mmoja na miezi sita sasa.

Wawili hao wamekuwa mahabusu gerezani kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana huku upelelezi wa kesi yao ukiwa bado haujakamilika.

Ndani ya muda waliokaa mahabusu wafanyabiashara hao wanaonekana kupitia mabadiliko mbalimbali na kuwafanya sasa waonekane tofauti na wakati ule kesi hiyo ilipokuwa ikianza.

Siku ya kwanza walipopanda kizimbani

Wafanyabiashara hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 19, 2017, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Siku hiyo, licha ya kukabiliwa na kesi walionekana ni watu wenye afya njema (mwonekano wa nje), maana licha ya kimuonekana kuonekana ni watu wenye umri mkubwa lakini walionekana imara, wenye nguvu na wenye nyuso ang’avu.

Rugemalira

Licha ya umri wake kuwa mkubwa, lakini alikuwa nadhifu kuanzia mavazi mpaka mwili kwa jumla.

Rugemalira ambaye kiumbo ni mrefu na mwenye mwili wa wastani, hakuwa mnene lakini pia hakuwa mwembamba bali alikuwa na mwili wa wastani, mwenye kitambi cha kawaida maana hakikuwa kikubwa kulinganisha na alivyokuwa mwenzake, Sethi.

Siku hiyo alivaa suruali aina ya ‘kadeti’ ya rangi ya khaki, akiwa ameifunga kwa mkanda mweusi na kuifanya ikae sawasawa kiunoni. Shati la mikono mifupi, lenye rangi nyeupe iliyofifishwa na michirizi mingi ya rangi za bluu na njano, alikuwa pia amelichomekea vema ndani ya suruali.

Shingoni mwake akining’iniza rozari, huku kwenye mfuko wa shati akiwa ameipachika kalamu yenye mfuniko mweusi. Miguuni alivaa viatu vya wazi vya mikanda vyenye rangi ya kahawia.

Kichwa chake kilifunikwa na nywele fupi mchanganyiko wa nyeupe (mvi) na nyeusi kwa uwiano uliokaribiana. Hakuwa na ndevu kabisa, alikuwa amenyoa zote.

Usoni alionekana mchangamfu na mara kadhaa akiwa anatabasamu na kuangaza macho ndani ya chumba cha mahakama, kuwaangalia waliokuwamo wakiwemo wapiga picha.

Namna alivyokuwa akipiga hatua katika kutembea ilidhirisha pasi na shaka kuwa alikuwa timamu kimwili yaani akionekana kuwa na nguvu au uimara wa mwili.

Hali hiyo ilidhihirishwa na jinsi alivyokuwa na uwezo wa kunyumbulika kiurahisi.

Kwa mfano siku hiyo walipotolewa mahabusu, kupelekwa katika chumba cha mahakama, askari polisi waliwaamuru kuchuchumaa kwa muda mfupi kabla ya kupelekwa mahakamani kusomewa mashtaka. Aliweza kufanya hivyo mara moja na kwa urahisi bila tabu, tofauti na mwenzake, Sethi.

Sethi

Siku hiyo hakuwa mchangamfu kama alivyokuwa Rugemalira, bali usoni alionekana mwenye mawazo, huku muda mwingi akiwa ameinamisha uso wake chini, akiunyanyua mara moja moja kwa wastani wa sekunde zisizozidi tatu na kuendelea kuinama.

Hata hivyo, kimwili alionekana kuwa imara, kwa jinsi alivyokuwa akitembea vema katika hali iliyoonesha kuwa hakuwa na tatizo kimwili.

Sethi ambaye ni mfupi kwa kimo, alikuwa mnene na mwenye kitambi kikubwa na mashavu yaliyojaa. Siku hiyo wakati walipoamriwa na askari polisi kuchuchumaa kabla ya kupelekwa katika chumba cha mahakama kusomewa mashtaka yao alionekana kupata shida sana kufanya hivyo.

Alijaribu mara kadhaa kuchuchumaa kama mwenzake Rugemalira alivyokuwa amefanya, lakini alishindwa. Haikuweza kufahamika kama kitambi kile ndicho kilikuwa kikwazo ama alikuwa na sababu nyingine pengine za kiafya. Badala yake aliamua kupiga magoti.

Siku hiyo alivaa suruali ya rangi nyeusi na shati jeupe la mikono mirefu lililokuwa likining’inia mwilini (hakuwa amechomekea). Miguuni alivaa viatu vya ngozi vya kufunika vyenye rangi nyeusi huku mkononi akiwa ameshikilia koti fupi la rangi ya kijivu.

Kichwani kama kawaida yake alikuwa amefunga kitambaa cheusi kikubwa kilichokunjwa kwa umaridadi na kuonekana kama kofia maalumu, huku mashavu yake na kidevu vikiwa vimefunikwa kwa ndevu nyeusi tii.

Siku hiyo walisomewa mashtaka sita ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, kujipatia fedha kwa udanganyifu, uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh358 bilioni. Julai 3, 2017, waliongezewa mashtaka mengine sita na kufikia mashtaka 12 yakiwamo ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana.

Sethi, ambaye Desemba 20, mwaka jana alifikishwa mahakamani akiwa amevalia shati jeupe na suruali nyeusi, kwa sasa amepungua kiasi kwamba hata kile kitambi kikubwa kilichokuwa kinajitokeza kwa urahisi hata anapovaa shati kubwa kiasi gani nacho kimepoteza ukubwa wake.

Mashavu yaliyokuwa yamejaa kwa sasa ni kama yamenyauka na kuonekana kama yamebonyea. Ndevu zake zile ndefu ambazo wakati ule zilikuwa nyeusi tii kwa sasa zote zimekuwa nyeupe pee.

Kesi yao bado haijaanza kusikilizwa ambapo upande wa mashitaka uliieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 3, 2019, itakapotajwa.