Marais waendelea kuwasili Tanzania kushiriki mkutano wa SADC

Rais wa Zambia, Edgar Lungu akipokelewa na waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar escsalaam leo kwa ajili ya mkutano wa 39 wa SADC unaotarajia kufanyika kesho. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Kesho Agosti 17, 2019 kunafanyika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dar es Salaam nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Marais wawili, Edgar Lungu wa Zambia na João Manuel Gonçalves Lourenço wa Angola wamewasilia Tanzania kuhudhuria Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Kuwasili kwa marais hao kunafisha idadi kufikia wanne  kati ya 16 wanaounda Jumuiya hiyo.

Mkutano huo unaoshirikisha nchi 16 za SADC unafanyika kuanzia kesho Jumamosi jijini Dar es Salaam ambapo Mwenyekiti wa mkutano huo ni Rais John Magufuli wa Tanzania.

Lungu ametua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Terminal III saa 7:41 mchana na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania wakiongozwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga.

Saa 8.09 mchana, Rais Lourenço wa Angola alitua katika uwanja huo na kupokelewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Viongozi wengine waliokuwapo uwanjani hapo ni; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bahungwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema.

Marais waliokwisha kuwasili nchini ni; Danny Faure wa Shelisheli na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi