VIDEO: Masha aibukia Vunjo kumnadi Kimei, Magufuli

VIDEO: Masha aibukia Vunjo kumnadi Kimei, Magufuli

Muktasari:

Ataka waliojiandikisha wajitokeze kupiga kura Keshokutwa Oktoba 28, 2020 kumchagua Rais, wabunge na madiwani

Moshi. Waziri wa wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrance Masha ameibuka katika dakika za lala salama za kampeni mkoani hapa akiwataka wananchi waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura, kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 28,2020.

Masha ameyasema hayo katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea ubunge katika Jimbo la Vunjo kupitia CCM, Dk Charles Kimei na kumuombea kura mgombea kupitia CCM, Dk John Magufuli.

"Ombi langu kwenu, Rais ametupatia sikukuu (Jumatano)  ili watu tupige kura, nawaombeni, tujitokeze kwa wingi tupige kura tumpate Dk Kimei, diwani wa  CCM na zaidi ya yote tumchague kaka yangu na rafiki yangu mpendwa, bosi wetu, Dk John Magufuli.

Akimzungumzia Dk Magufuli amesema, “ukweli ni kwamba, kazi ambayo ameifanya hapa nchini hakuna mfano."

Akizungumza wakati akiomba kura Dk Kimei, amesema anazo mbinu za kupata majibu ya changamoto na kero zinazowakabili wananchi wa Vunjo, ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara.

Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya amesema siasa za porojo zimepitwa na wakati na kuwasihi wananchi watoke Misri na kwenda Kanaani kwa kumchagua Dk Kimei na Dk Magufuli.

"Tunahitaji kumpata kiongozi mwenye hofu ya Mungu, muadilifu na mchapa kazi,  msifanye tena makosa, mchagueni  Dk Kimei kwa kuwa ni muadilifu, ana hofu ya Mungu na ni mchapakazi na ndiye mwenye majibu sahihi ya changamoto zenu," amesema Mabihya.