Masharti mapya vitambulisho vya machinga

Dar es Salaam. Wakati serikali ikiandaa masharti mapya kwa ajili ya vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo, Takukuru imebaini wizi wa mamilioni ya fedha katika mradi huo mkoani Mtwara.

Vitambulisho hivyo vya mwaka mmoja, ambavyo Rais John Magufuli alitaka wapewe wafanyabiashara wenye mtaji usiozidi Sh4 milioni kwa kulipia Sh20,000, vimeisha muda wake Desemba 31 mwaka jana, na hivyo wanatakiwa wapewe vipya kwa ajili ya mwaka 2020.

Lakini haitakuwa rahisi kuvipata kama ilivyokuwa mwaka wa kwanza, kwa mujibu wa katibu mkuu wa Tamisemi.

Uchunguzi wa Mwananchi katika wilaya na mikoa umebaini kuwa tayari Ofisi ya Rais - Tamisemi imeshawaandikia barua watendaji husika kuwaeleza kuhusu kusitisha ugawaji wa vitambulisho vya awali, ambavyo vilikuwa na namba pekee na alama nyingine za siri.

Kutobandikwa picha, kulitoa mwanya kwa wafanyabiashara hao, maarufu kwa jina la wamachinga, kubadilisha vitambulisho hivyo na hata wasiostahili kuvipata kwa lengo la kuvitumia kuuza bidhaa bila ya kulipa kodi baada ya Rais John Magufuli kuagiza kuwa yeyote atakayemilikishwa nyaraka hiyo asibughudhiwe na maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Tamisemi imewaeleza wakuu wa wilaya wasitishe ugawaji wa vitambulisho hadi pale watakapopewa maelezo mengine.

Katibu mkuu wa Tamisemi, Joseph Nyamhanga aliiambia Mwananchi kwamba Serikali imeelekeza kusitishwa kwa ugawaji wa vitambulisho vya zamani na kwamba vitambulisho vipya vinaandaliwa.

“Tunaandaa vitambulisho vipya kwa mwaka huu kwa sababu vilivyopo ni vya mwaka 2019 na muda wake ulimalizika Desemba mwaka jana. Kwa hiyo haviwezi kutumika mwaka huu,” alisema Nyamuhanga.

Alisema kwa kuzingatia uzoefu walioupata mwaka jana, vitambulisho vipya vitakuwa na masharti na mojawapo ni kuwekwa picha ya muhusika, ili kuepusha kile alichokiita matumizi yasiyofaa kwa waliogawiwa.

“Vitambulisho vya awali havikuwa na alama yoyote ya muhusika, hivyo kutoa mwanya kwa waliopewa kupeana bila utaratibu. Kwa hiyo vipya vitakuwa na picha,” alisema.

Kwa mujibu wa katibu huyo mkuu, kama ilivyokuwa mwaka jana vitambulisho vipya vitalipiwa Sh20,000.

“Malipo ni lazima. Huwezi kulipa Sh20,000 halafu ukatumia kitambulisho hicho milele. Ilielezwa tangu mwanzo kwamba kila mwaka kutakuwa na malipo kwa wanaovihitaji,” alisema.

Nyamhanga hakutaja masharti mengine kwa maelezo kuwa bado wanaandaa utaratibu mzuri utakaodhibiti vitambulisho hivyo.

Jana Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Richard Kayombo aliliambia gazeti hili kuwa fedha zilizokusanywa kwa kuuza vitambulisho hivyo ni zaidi ya Sh30.4 bilioni.

Vitambulisho 67,000 vya wamachinga vilitolewa Desemba 10, 2018 na Rais John Magufuli akisema kila atakayekuwa na kitambulisho cha aina hiyo asibughudhiwe katika eneo atakalokuwa akifanyia shughuli zake.

Rais aliamua kutoa vitambulisho hivyo baada ya serikali za mikoa na wilaya kushindwa kumpa utaratibu wa jinsi wafanyabiashara hao wadogo wanavyoweza kufanya kazi katika mazingira yasiyo na bughudha.

Katika kipindi cha kuelekea kutolewa kwa vitambulisho hivyo, wafanyabiashara hao walikuwa wakihamishiwa nje ya miji, lakini Rais akazuia, akisema kazi hiyo ifanyike wakati wameshaandaliwa maeneo mazuri.

Pia walikuwa wakipambana na maofisa wa TRA na askaji wa miji na majiji kwa ajili ya tozo za ushuru na kodi, lakini Rais akasema wasilipishwe tozo yoyote.

Hali ilivyo

Katika baadhi ya mikoa, Mwananchi imebaini vitambulisho hivyo vimegawiwa vyote na kubakia huku wakuu wa wilaya au mikoa wakieleza kuwa wanasubiri utaratibu mwingine.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Nnunduma alisema katika wilaya yake awamu ya kwanza walipewa vitambulisho 2,500 na walivigawa vyote.

Alisema awamu ya pili walipewa vitambulisho 4,000 na waligawa 2,000 tu.

“Tumeletewa barua tusiendelee kuvigawa maana muda wake wa matumizi umekwisha, ni vya mwaka mmoja. Kwa sasa tumesitisha hadi tutakapopewa utaratibu mwingine,” alisema Nnunduma.

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odinga alisema walipokea vitambulisho 8,250 kwa awamu mbili na wamegawa kwa wafanyabiashara 7,304 hivyo kubakiwa na vitambulisho 946.

Alisema bado wanasubiri uamuzi ya Serikali kuhusu vitambulisho hivyo, iwapo vitatolewa vingine ama vitaendelea kutumika vilivyopo.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi alisema waligawa kwa machinga wapatao 7, 500 katika wilaya hiyo na kwamba kila kata wana daftari ambalo linajumuisha wafanyabiashara wote waliopewa.

“Fedha zote tulishawasilisha kwa vile vilivyouzwa. Tunavifanyia uhakiki vitambulisho, kujua kwamba vililipiwa ama kuna wengine walivipata kinyemela ama vipi,” alisema.

Mkoani Lindi, katibu tawala msaidizi wa mkoa huo, Majdi Myao alisema vitambulisho 35,291 viligawiwa kati ya 65,000 vilivyotolewa.

Alisema kila wilaya ilipwa vitambulisho 5,000. Alisema vitambulisho katika wilaya zote vilimalizika isipokuwa Liwale vilibaki 44.

Alisema mgawo wa awamu ya pili vilitolewa vitambulisho 40,000, na kwamba asilimia 54.3 ya vitambulisho walivyopewa vimewafikia walengwa wamebaki na vitambulisho 29,709 sawa na asilimia 45.7.

Mkoani Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Danile Chongolo alisema katika wilaya yake walipewa awamu mbili na vitambulisho vyote vilitolewa kwa wajasiriamali vikaisha.

“Vilitolewa awamu ya kwanza vikaisha, vikaletwa vingine pia vikamalizika,” alisema.

Mkoani Kilimanjaro, ofisa habari wa mkoa, Shaban Pazi alisema walipatiwa vitambulisho 65,000 na viligawanywa vyote, wakati Arusha viligawiwa vitambulisho 80,000 kati ya 125,000.

Katibu tawala wa mkoa, Richard Kwitega alisema idadi kubwa ya vitambulisho imetolewa na bado takwimu zinakusanywa.

Mkuu wa wilaya ya Monduli, Idd Kimanta alisema ugawaji vitambulisho uliratibiwa na ofisa biashara wa halmashauri.

“Tunakwenda vizuri wajasiriamali wengi wamepatiwa vitambulisho na vinawasaidia katika biashara zao,” alisema.

Imeandikwa na Elizabeth Edward, Sharon Sauwa, Rachel Chibwete, Haika Kimaro, Mwanja Ibadi na Mussa Juma