Mashirika matano ya umma yatajwa na CAG kuwa na upungufu

Muktasari:

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2019  imebaini upungufu  kadhaa katika mashirika ya umma matano kati ya 40.

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2019  imebaini upungufu  kadhaa katika mashirika ya umma matano kati ya 40.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashirika hayo ni Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Shirika la Posta Tanzania, Shirika la Nyumba la Taifa, Bohari Kuu ya Dawa na Mamlaka ya Kesi za Manunuzi ya Rufaa.

Upungufu huo ni kukosekana kwa ushiriki wa vitengo vyote katika uandaaji wa bajeti, kutokuwepo kwa uhusiano kati ya mpango mkakati wa taasisi na bajeti, na kutokuwepo kwa taarifa za kutosha za utekelezaji na ufuatiliaji wa bajeti.

Katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ripoti ya CAG imesema kuwa ilinunua magari kwa gharama iliyokuwa juu ya bajeti kwa Sh226.57 milioni.

“Hakukuwa na bajeti ya kiasi kilichoongezeka kwenye manunuzi hayo kinyume cha aya ya 224 ya kanuni za fedha za Bohari Kuu za mwaka 2011 ambazo zilitaka kabla ya kufanya maamuzi yoyote lazima mkurugenzi ahakikishe matumizi yanayopendekezwa yapo katika bajeti iliyoidhinishwa na mpango wa manunuzi wa mwaka,” ilieleza ripoti hiyo.

Kwa upande wa Shirika la Nyumba la Taifa, ripoti ya CAG imesema kwamba mchakato wa kuandaa mpango wa utekelezaji wa mwaka haukuzingatia mpango mkakati wa taasisi kwa kipindi hicho.

“Kwa mfano, katika mpango mkakati, Shirika la Nyumba lilionyesha litakusanya Sh240 bilioni kwa mwaka 2018/2019 lakini katika mpango kazi wake kwa mwaka huo lilionesha litakusanya Sh167.7 bilioni,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti ya CAG imesema Shirika la Posta Tanzania (TPC)  iliidhinisha Sh1.1 bilioni  kwa ajili ya kukarabati majengo ya ofisi.

Hata hivyo, bajeti na mpango kazi wa mwaka havikuwa na fedha hizo zilizotegwa kwa ajili ya shughuli za ukarabati huo wa ofisi katika mikoa sita.

“Menejimenti haikuandaa makisio ya bei (BOQ) ambapo ingeweza kutumika kama mwongozo wa gharama ya ukarabati kwa kila jengo la kila mkoa,” inaeleza ripoti hiyo.

Lakini kwa upande wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, ripoti ya CAG inataja upungufu kuwa ni kosekana kwa ushahidi wa ushirikishwaji wa kila idara katika mfumo wa uandaaji wa bajeti na bajeti kutoonesha vipaumbele na namna bora ya kutenga rasilimali fedha kwa shughuli za msingi za taasisi.

Pia ilibaini kutowepo kwa tathmini za kila robo mwaka zikionesha ni kwa namna gani malengo ya bajeti yamefikiwa.