Matarajio ya wanachama Chadema

Muktasari:

Wajumbe wa  mkutano mkuu wa Chadema wamesema  chama hicho kushika Dola ni miongoni mwa matarajio yao baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti  leo Alhamisi Desemba 19, 2019.

Dar es Salaam. Wajumbe wa  mkutano mkuu wa Chadema wamesema  chama hicho kushika Dola ni miongoni mwa matarajio yao baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti  leo Alhamisi Desemba 19, 2019.

Katika uchaguzi huo ulioanza jana asubuhi na kuhitimishwa leo Alfajiri, Freeman Mbowe amechaguliwa kuwa mwenyekiti huku Tundu Lissu akichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti (Bara) na Said Issa Mohammed (Zanzibar).

“Tuna timu mpya ambayo inaonyesha dira kukamata nchi mwakani. Wanachama wana imani kubwa na viongozi hawa ambao wengine ni  wapya. Chadema ipo imara wengi walidhani uchaguzi huu wa ndani  ungekwama lakini umekwenda vizuri, “ amesema  Seme Mawingo  kutoka kanda ya Nyasa.

Suzana Mgonukulima kutoka Iringa amesema, “ninaiona njia nyeupe Chadema kushika Dola endapo tu uchaguzi utakuwa huru na wa haki bila bughudha.”

Kwa upande wake, Ahmed Rashid kutoka Unguja amesema ana matarajio makubwa na safu ya uongozi, “viongozi hawa watatufikisha mbali kwa kweli, ni watu makini.”

Safu ya viongozi wa chama hicho itahitimishwa leo atakapochaguliwa katibu mkuu na naibu katibu mkuu wa Bara na Zanzibar.