Matukio makubwa ya uhalifu, barabarani yapungua Tanzania

Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Tanzania, Robert Boaz

Muktasari:

Jeshi la Polisi Tanzania limetoa tathimini ya mwenendo wa matukio ya makosa makubwa ya uhalifu yakionyesha kupungua kwa asilimia 3.2 katika kipindi cha Januari hadi Februari 2020 ukilinganisha na kipindi hicho mwaka 2019.

Dodoma. Jeshi la Polisi Tanzania limesema matukio makubwa ya uhalifu yaliyoripotiwa katika kipindi cha Januari na Februari 2020 yamepungua kwa asilimia 3.2 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2019.

Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Tanzania, Robert Boaz amesema leo Jumamosi Machi 28 2020 kuwa katika kipindi cha Januari hadi Februari 2020 matukio makubwa yaliyoripotiwa yalikuwa ni 9,263 ukilinganisha na 9,572 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2019.

“Huu ni upungufu wa matukio 309 sawa na asilimia 3.2,” amesema Boaz.

Aidha amesema makosa ya usalama wa barabarani makubwa katika kipindi cha Januari na Februari 2020 ni 425 ukilinganisha na matukio 533 yaliyoripotiwa katika kipindi hicho mwaka 2019.

Kamishna Boazi amesema huo ni upungufu wa matukio 108 sawa na asilimia 20.3.