Matumizi ya karatasi utoaji dawa vituo vya afya marufuku

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile, amepiga marufuku matumizi ya karatasi katika utoaji wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini na kwamba kuna mianya ameibaini ya upotevu wa dawa vituoni.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania, Dk Faustine Ndugulile amepiga marufuku watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya kutumia karatasi kama njia ya kuidhinisha maombi ya dawa.

Dk Ndugulile ametoa marufuku hiyo mara baada ya kubaini mianya ya upotevu wa dawa za Serikali katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini alipokuwa ziarani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi).

"Kuanzia sasa ni marufuku  kutumia karatasi za daftari kuomba dawa kutoka idara moja kwenda nyingine, tuandae fomu maalum za maombi,” amesema Dk Ndugulile.

Ameagiza dawa zote zinazopatikana katika vituo vya kutolea huduma ziwekwe kwenye fomu za maombi (reiquizitation form) huku zikionyesha jina la  aliyeomba pamoja na kusaini kuthibitisha maombi yake ya dawa.

Amesema pia, mtu au idara ya famasia inayopokea maombi hayo anatakiwa kuyahakiki maombi na kusaini fomu hiyo.

“Ni marufuku kwa mtu wa famasia kujiongezea dawa kwa maneno ya mdomo au kuambiana, na atakayepokea dawa hizo pia anatakiwa aandike jina lake na kusaini,” alisema.

Aliendelea  kusema, “Serikali imewekeza nguvu kubwa sana katika upande wa dawa, lakini pia nyie wataalam ambao mnasimamia mnatakiwa kuhakikisha mnaweka kumbukumbu zenu sahihi ili kudhibiti mianya ya upotevu wa dawa,”

“Hapa ninapata mashaka kuwa kuna upotevu wa dawa za Serikali tujirekebishe na kuhakikisha tunatunza vizuri kumbukumbu zetu,” amesema Dk Ndugulile.

Kwa upande  mwingine, Dk Ndugulile ameagiza uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanaweka mifumo ya TEHAMA katika kusimamia maombi ya dawa.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) Dk Jumanne Karia amesema wamepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyatekeleza mara moja.

“Tunamshukuru kwa maelekezo yako, tutaendelea kuunga mkono Wizara ya Afya na tutatekeleza maelekezo uliyoagiza,” amesema Dk Karia.