Mauaji, ukatili watanda mwaka mpya

Moshi/mikoani. Msimu wa sikukuu unajulikana kwa kuweka familia pamoja kuimarisha upendo, lakini mwaka huu umemalizika vibaya kwa baadhi; mauaji, kujeruhiana, kujinyonga ndio yametawala tarehe za mwanzo za mwaka.

Mkoani Kilimanjaro, polisi wanamsaka mama na mtoto wa miaka 12, ambaye anatuhumiwa kumuua kwa jiwe mpenzi wa mama yake mzazi aliyetajwa kuwa ni Serafin Mrema (29), wakati mkoani Shinyanga, polisi aliyejulikana kwa jina moja la Kazimili (28) alikatwa sehemu za siri na mke wake kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa kimapenzi.

Na mkoani Mwanza, Benedictor Gogogo (48), mkazi wa kijiji Cha Itabagumba wilayani Sengerema, anaendelea kuuguza jeraha tumboni baada ya kuchanwa na mkewe katika ugomvi kuhusu matumizi ya Sh10,000.

Hayo ni matukio ambayo taarifa zake zilitoka juzi.

Jana kutoka mkoani Kagera habari zinasema kuwa baba wa kambo anatuhumiwa kumuua mtoto wa miaka mitatu, Caren Crispin kwa kumkata kichwani na mkononi katika ugomvi wa kifamilia.

Tukio jingine limetokea mkoani Tabora ambako mtu mmmoja amejinyonga kwa upande wa khanga ya mkewe na taarifa za awali zinasema uamuzi huo umetokana na wivu wa kimapenzi.

Tukio jingine la polisi kuuawa mkoani Kilimanjaro na mwingine wa mkoani Tabora kujinyonga, hayahusiani na masuala ya kifamilia.

Wawili wajinyonga

Mkoani Tabora, polisi imetangaza kuanza kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaosababisha wengine kujinyonga baada ya watu wawili kuchukua uamuzi huo.

Katika tukio la kwanza, mwalimu wa Shule ya Msingi Ikongolo wilayani Uyui, Basil Sungu (39) amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kipande cha kitenge cha mke wake.

Mwili wa Sungu ulikutwa chumbani kwake ukiwa umening’inia darini Desemba 31 mwaka jana.

“Uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea ingawa taarifa za awali zinadai kuwa kabla ya kifo chake, marehemu alikuwa na mgogoro wa kifamilia na mke wake Theresia Ali,” alisema kamanda wa mkoa.

Pia mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la James Albert (22), mjasiriamali na mkazi wa kata ya Chemchem Manispaa ya Tabora, alikutwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia mkanda wa begi.

Polisi wamesema wanaendelea na upelelezi kubaini kwa nini marehemu aliyekutwa akining’inia kwenye kenchi za paa sebuleni kwake alichukua uamuzi huo wa kujinyonga.

Akizungumzia matukio hayo, kamanda wa polisi mkoa, Barnabas Mwakalukwa alisema uamuzi huo unalenga kukabiliana na ongezeko la matukio ya watu kujinyonga. “Vitendo vya watu kujinyonga havifurahishi na vinatia simanzi hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya wahusika ni wanandoa ambao vifo vyao husababisha shida kwa watoto, mke au mme anayebaki,” alisema Kamanda Mwakalukwa

“Tutaanza kuwasaka wale wote wanaosababisha wenzao kujinyonga ili sheria ichukue mkondo wake kwa sababu wanasababisha simanzi kwa familia husika.”

Katika tukio jingine mkoani Kagera, polisi wanamshikilia Leonardi Kishenya kwa tuhuma za kumuua kwa kitu chenye nchi kali, mtoto wa miaka mitatu, Caren Crispin mkazi wa kijiji cha Katorelwa wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi alisema tukio hilo lilitokea usiku wa mkesha wa mwaka mpya.

Alisema siku ya tukio, baba huyo wa kambo na mkewe Domina Andrew walikuwa wametoka kwenye starehe usiku.

“Waliporejea nyumbani waliingia kwenye ugomvi uliomfanya mwanamke kukimbia na kulala kwa majirani akimwacha mume wake ndani na mtoto,” alisema Kamanda Malimi.

“Lakini aliporudi nyumbani kesho yake alimkuta mtoto ameuawa kwa kukatwa kichwani na mkono wa kushoto na kisu.”

Alisema mama huyo alitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ambao walifikisha suala hilo kituo cha polisi na kufanikisha kumtia mbaroni mtuhumiwa aliyetoroka baada ya mauaji hayo.

Polisi auawa Kilimanjaro,

Katika tukio jingine mkoani Kilimanjaro, polisi wanawasaka watu wanaotuhumiwa kumuua kwa kumchoma visu polisi anayejulikana kwa jina la Living, ambaye alikuwa ametoroka lindo na kwenda kunywa pombe na askari mwenzake.

Kaimu Kamanda James Manyama alisema siku hiyo ya Desemba 22 mwaka jana, saa 9:00 usiku, polisi hao waliokuwa lindo kituoni kwao wilayani Same, walikwenda kunywa nyumbani kwa mwanamke mmoja Mtaa wa Mnadani na kuficha silaha kwenye magari mabovu kituoni.

“Baadaye Askari namba Living alikutwa peke yake eneo hilo akiwa na jeraha huku akitokwa na damu, huku watuhumiwa wakiwa wameshakimbia,” alisema.

Alisema chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa na wanawasaka wahusika, huku akiomba ushirikiano wa wananchi.

Kuhusu polisi aliyetoroka lindo pamoja na marehemu, kamanda huyo alisema atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Mama, mtoto wasakwa

Tukio linaloendelea kugonga vichwa ni la mtoto wa miaka 12 kutuhumiwa kumuua mpenzi wa mama yake kwa kumpiga na jiwe. Mtoto na mama wanasakwa na polisi, kamanda Manyama alisema jana.

Tukio hilo lilitokea Desemba 25 mwaka jana barabara ya Kibosho.

“Taarifa ambazo zinachunguzwa ni kuwa marehemu alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mama wa mtuhumiwa. Siku ya tukio mtuhumiwa alimkuta Serafin akiwa chumbani kwa mama yake mzazi,” alidai.

“Mtuhumiwa alimfukuza marehemu kutoka chumba cha mama yake na wakati anatoka nje ndipo alimrushia jiwe lililompata kichwani na kuanguka chini na kupoteza fahamu,” alieleza.

“Upelelezi zaidi unaendelea ikiwa ni pamoja na kumsaka mtuhumiwa ambaye ametoroka baada ya tukio hilo na mama wa mtuhumiwa ambaye naye aliondoka nyumbani hapo baada ya tukio.”

Kamanda huyo alisema mwanamume huyo, ambaye alikuwa akijishughulisha na kilimo, alipelekwa Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi ambako alifariki wakati akipatiwa matibabu.

Ingawa Kaimu kamanda huyo hakueleza iwapo uchunguzi wa mwili wa marehemu (post-mortem) ulifanyika, taarifa kutoka vyanzo vingine zinasema ulifanyika.

“Post-mortem (uchunguzi wa kiini cha kifo) ilifanyika kabla ndugu hawajachukua mwili kwenda kuzika na ilibainika kiini cha kifo ni kupigwa na kitu butu kichwani,” alidokeza ofisa mmoja wa polisi.

Mama mdogo, majirani wasimulia

Tukio hilo bado limeendelea kuibua utata hasa ni wakati gani marehemu alipigwa jiwe ama ni wakati akitoka chumba cha mama wa mtuhumiwa au aliporejea kutoka baa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Esther Jeremia, ambaye ni mama mdogo wa marehemu na jirani, alidai siku hiyo mwanaume huyo aliingia chooni na alipotoka ndipo alipoanza kumrushia mawe na jiwe moja likampata kichwani.

“Alianguka chini huku akivuja damu nyingi. Watoto waliokuwapo eneo hilo, walipiga kelele na kwenda kuita ndugu wanaoishi jirani,” alisema Esther.

“Walimpeleka zahanati ya jirani na kuambiwa wampeleke Mawenzi. Hili si tukio la kwanza kwa kuwa waliwahi kugombana na akampiga tena na jiwe lakini marehemu alimkamata na kumpiga sana.”

Alisema mara kadhaa wawili hao walikuwa wakigombana na chanzo kikubwa kilikuwa ni uhusiano wa kimapenzi wa mama na kijana huyo.

“Mtoto alikuwa akimuonya huyo kaka na mama yake waache mahusiano ya kimapenzi kwa madai kuwa baba yake bado yupo hai, na hilo lilikuwa likimfanya kuwafuata hadi baa,” alisema.

Edward Mrema, ambaye ni ndugu wa marehemu, alisema alipata taarifa ya ndugu yake kupoteza fahamu akiwa katika shughuli zake.

Mrema alisema alifika eneo hilo na kukuta tayari amepelekwa hospitali na akaenda.

“Alifariki wakati anapatiwa huduma ya kwanza Mawenzi, tulienda polisi na kuonana na mkuu wa kituo Moshi na alituma askari eneo la tukio na baadaye polisi walituambia tumzike ndugu yetu, wakati taratibu nyingine zinaendelea,” alisema.

“Baada ya kufariki Hospitali walituambia kuwa kifo kimetokana na jiwe alilopigwa, tumeshamzika juzi Jumanne, na sasa tunasubiri taarifa nyingine za polisi, ili kujua walikofikia na uchunguzi wao.”

Imeandikwa na Daniel Mjema, Janet Joseph na Florah Temba (Moshi), Robert Kakwesi (Tabora), Alodia Dominick (Kagera)