Maumivu ya mkono yasababisha Mdee kushindwa kufika mahakamani

Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee, akichangia bungeni jijini Dodoma leo baada ya Spika wa Bunge kutoa taarifa kwa wabunge ya mabadiriko ya uendesha wa vikao vya Bunge kutoka na ugonjwa wa virus vya corona. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Mdee anakabiliwa na shtaka la kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli na alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 10, 2017

Dar es Salaam. Faris Lupomo ambaye ni mdhamini wa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshtakiwa huyo ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana ana maumivu makali katika mkono wake uliovunjika.
Mdee anakabiliwa na shtaka la kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli na alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 10, 2017.
Mdhamini huyo amesema hayo baada ya Wakili wa Serikali, Silyvia Mitanto kueleza mahakamani leo Jumatano Aprili Mosi, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutolea uamuzi lakini mshtakiwa hayupo mahakamani hapo.
Kutokana na maelezo hayo Lupomo aliieleza mahakama hiyo kuwa Mdee alikuwa anasafiri akitokea mkoani Dodoma kuja jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuhudhuria kesi hiyo pamoja na kliniki kwa ajili ya mkono wake uliovunjika.
"Kwa bahati mbaya akiwa safarini akitokea Dodoma kuja Dar es Salaam mkono wake umeshtuka na anasikia maumivu makali sana hivyo ameshindwa kufika mahakamani,"alieleza Lupomo.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba aliahirisha shauri hilo hadi Aprili 28, 2020 kwa ajili ya kutolewa uamuzi.
Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Mdee alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa, ‘anaongea hovyo, anatakiwa afungwe breki,’ kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.